Serikali imefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuweka mfumo madhubuti wa huduma za dharura na ajali kuanzia ngazi ya Taifa hadi wilaya ambapo matokeo ya uwekezaji huo ni kupunguza vifo kwa 40% ndani ya hospitali na kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma za dharura nchini.
Akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/2024 kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa mapinduzi hayo ni makubwa kufanyika katika sekta ya Afya tangu Tanzania ipate Uhuru.
Waziri Ummy amesema, Wizara imeendelea kukamilisha ujenzi wa majengo 23 ya kutoa huduma za dharura (EMD) katika Hospitali Maalum, Kanda na Mikoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba. “Hadi kufikia Machi 2023 jumla ya EMD 15 zilikuwa zimekamilika na zimeanza kutoa huduma. Kukamilika kwa ujenzi wa EMD kumeongeza idadi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, maalumu, na kanda zinazotoa huduma hiyo kutoka nane (8) mwaka 2021 na kufikia 38 kipindi cha mwezi Machi 2023”.
Aidha, Serikali ya awamu ya sita kupitia OR-TAMISEMI imewezesha ujenzi wa majengo ya EMD 80 katika ngazi ya Hospitali za Halmashauri. Jumla ya majengo ya kutoa huduma za dharura (EMD) yamefikia 118 kutoka 8 mwaka 2021. ‘Haya ni mapinduzi makubwa katika Sekta ya Afya hapa Tanzania tangu uhuru kwa Serikali kuweka mfumo madhubuti wa huduma za dharura kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya. Matokeo ya uwezekaji huu yatapunguza vifo ndani ya Hospitali kwa asilimia 40 na kuokoa maisha ya wananchi wanaohitaji huduma za dharura’.
Aliongeza kusema kuwaWizara imeendelea kukamilisha ujenzi wa wodi 45 kwa ajili ya wagonjwa mahututi na wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) katika Hospitali ngazi ya Taifa, Maalum, Kanda na Mkoa na kuziwekea vifaa na vifaa tiba, ambapo hadi kufikia Machi 2023 jumla ya ICU 33 zilikuwa zimekamilika na zimeanza kutoa huduma.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya ICU kutaongeza idadi ya vitanda vya ICU kutoka vitanda 258 vilivyokuwepo na kufikia jumla ya Vitanda 1,000. “Uwekezaji huu uliofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan utaokoa maisha ya wananchi wengi zaidi ndani ya Hospitali kwa asilimia 20 hadi 30”.
Hata hivyo alisema ,Wizara imefanya tathmini ya magari ya wagonjwa (Ambulance)nchini ambapo jumla ya magari 595 kati ya magari 761 yaliyopo yanafanya kazi na 221 yapo katika hatua mbalimbali za matengenezo. Serikali kupitia Wizara ya Afya na OR TAMISEMI imekamilisha ununuzi wa magari ya kubebea wagonjwa 727 ambapo hadi sasa jumla ya magari 77 yamewasili nchini.“Uwepo wa magari ya wagonjwa (ambulance) utasaidia kusafirisha wagonjwa mbalimbali wakiwemo akinamama wajawazito kwa wakati na kuokoa maisha yao na vichanga vyao. Magari haya pia, yatasaidia huduma za uokoaji na huduma kwa wahanga wa ajali katika barabara kuu na kuwasafirisha kwa wakati huku wakipatiwa huduma wakati wakiwa njiani”.
Kwa upande wa huduma za matibabu ya Kibingwa na ubingwa Bobezi Waziri Ummy alisema kuwa ,Wizara imeendelea kuboresha na kuimarisha huduma za matibabu ya Kibingwa na Ubingwa bobezi nchini kwa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi kwa kuendesha kambi mbalimbali za matibabu ya mkoba ikiwa pamoja na huduma za ushauri, upasuaji na matatizo mbalimbali.
Alisema katika kipindi cha Julai 2022 hadi machi 2023 jumla ya wagonjwa 80,018 walihudumiwa kupitia mpango huo “mpango huo umewezesha wananchi kupata huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa gharama nafuu, Serikali itaendelea kuimarisha huduma hizi ili ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kugharamia huduma husika”.
About The Author
Last modified: May 30, 2023