Azindua Kanzidata ya madereva wa malori nchini
Na Beatrice Kaiza
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepokea hundi ya sh. milioni 100 kutoka kwa wanachama cha wamiliki wa Malori nchini (TATOA) ikiwa ni mchango wao kwa waathirika wa maafa ya mafuriko huko Katesh, wilayani Hanang, mkoani Manyara.
Waziri Mkuu amepokea hundi hiyo leo (Alhamisi, Desemba 14, 2023) katika hafla ya uzinduzi wa kanzidata ya madereva wa malori nchini, jijini Dar es Salaam ambayo imeandaliwa na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA).
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu amesema azma ya Serikali ya awamu ya Sita ni kuendeleza sekta hiyo kwa kuboresha miundombinu ili iweze kuharakisha ukuaji wa uchumi. “Hatua iliyofikiwa leo ni kuhakikisha makao makuu ya mikoa yote inafikika kwa lami na shoroba zote za Kusini, Kati na Kaskazini kuelekea nchi za jirani za Kenya, Kongo, Malawi na Zambia zinapitika bila shida.
“Serikali tayari imekamilisha ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa km. 2,183.82 na km. 14,348 za changarawe. Licha ya hayo imekuwa ikiendelea na matengenezo ya kawaida ili kuzifanya barabara zetu ziweze kupitika wakati wote” amesema.
Sambamba na maboresho hayo ya barabara, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (SGR) unaoambatana na uundaji wa vichwa 17 vya treni, uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga na kwenye maziwa makuu ya Victoria, Tanganyika na Nyasa ambapo muda wa kugomboa mizigo bandarini umepungua kutoka siku 14 hadi siku sita.
“Uimarishwaji wa sekta hizi haulengi kuua usafirishaji wa malori kwani ujenzi upanuzi wa bandari zetu, utaleta mizigo mingi zaidi na kazi ya usafirishaji itafanywa na ninyi,” amesema.
Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa hafla hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, aliwapongeza viongozi wa TATOA kwa ubunifu wao mkubwa wa kuamua kuandaa kanzidata hiyo.
Amesema Serikali inao mfumo wa kusajili madereva ulioko chini ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ambao umeshasajili madereva 19,709 wakiwemo wa mabasi na malori. “Kanzidata hii itatumiwa pia na Serikali kufuatilia mwenendo wa madereva wa malori”.
About The Author
Last modified: December 14, 2023