Visit Sponsor

Written by 3:58 pm KITAIFA Views: 41

WAZIRI MBARAWA AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI WA MISRI KWENYE MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI

Na Beatrice Kaiza

Waziri wa uchukuzi profesa Makame Mbarawa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini Misri kuwekeza nchini Tanzania kwenye miundo ya usafirishaji hatua ambayo itasaidia nchi kuleta mageuzi ya haraka kiuchumi nchini na nchi zinazotegemea bandari za Tanzania kupitisha mizigo yao.

Ameyasema hayo leo jijijni Dar es salaam wakati akifungua kikao cha kimkakati baina ya Taasisi kumi na nne zilizopo chini ya wizara ya uchukuzi na ujumbe wa wataalamu kutoka nchini misri ukiongozwa na waziri wa uchukuzi wa nchini Misri.

“Leo tumekutanika hapa, tumepata ugeni muhimu sana ambao unaongozwa na waziri wa uchukuzi, ambao umekuja kujifunza fursa gani za uwekezaji ambazo ziko hapa Tanzania na tumeeleza fursa mbalimbali ambazo wanaweza kuzipata katika Sekta ya Uchukuzi hapa nchini, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya Uchukuzi, ni Sekta ambayo serikali imepeleka pesa nyingi sana kuhakikisha kwamba Sekta ya Uchukuzi inakua kwasababu tunaamini Sekta ya Uchukuzi pamoja na miundombinu mingine ikikua na uchumi wa nchi utakua kwa asilimia kubwa na kwa haraka zaidi”

Waziri Mbarawa aliyataja maeneo ambayo yanayohitaji uwekezaji, ambayo ni pamoja na bandari ya Dar es salaam Gati namba 13,14,na 15 ambalo linahitaji kujengwa kwa kushirikiana na serikali ya misri ili kusaidia kupunguza foleni za meli bandarini hapo

“Maeneo ambayo wanaweza kuwekeza ni katika Bandari ya Dar es Salaam, tuna mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari namba 13,14 na 15 katika mfumo wa PPP kwaajili ya ushirikishaji wa Sekta binafsi, mradi huu ni muhimu kwasababu utafungua na kupunguza sana changamoto zinazotokana za meli zinazotokea kwenye meli yetu ya Dar es Salaam.”

Maeneo mengine ya uwekezaji kwenye miundombinu ya usafirishaji yaliyobainishwa ni pamoja na uwekezaji wa ujenzi wa gati la kushusha mafuta Tanga , ujenzi gati la mizigo Mtwara , ujenzi wa reli itakayoanzia Kailua mpaka mpanda , ujenzi wa reli Mtwara mpaka mbamba bay , na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo.

“Fursa nyingine ya dar es salaam kwaajili ya kujenga Gati kubwa kwaajili ya kuteremshia mafuta ambayo pia wataliona eneo hilo na watafanya maamuzi”

“Mtwara kuna fursa ya Reli inayotoka Mtwara- Bambabei yenye urefu wa Km 1000 na mpaka sasa tunatafuta wawekezaji, pia kuna maeneo ya Tanga hadi Uganda, tuna mradi wa Reli na tunatafuta wawekezaji kwaajili ya ujenzi wa Reli kutoka Kaliua- Mpanda kwaajili ya ujenzi wa Bandari ya Karema” Alisema Waziri Mbarawa.

Kwa upande wake waziri wa uchukuzi wa Misri, lutenant general Kamel Alwazeer,amesema kuwa, Misri ipo tayari kushiriki na Afrika hususani Tanzania katika sekta ya usafirishaji kuanzia teknolojia , bunifu na ujenzi wa miundodombinu ili kurahisisha shughuli za kiuchumi baina ya mataifa Haya mawili na Dunia kupitia sekta ya uchukuzi.

“Katika kuelekea upande wa kisiasa tunatakiwa tuboreshe ushirikiano wetu pia tuendeleze mfumo mzima wa biashara kati ya nchi zetu ambayo utapelekea kupatikana kwa miradi mikubwa ndani ya nchi, kuna umuhimu wa kuongeza kujenga miundombinu ya ziada ya bahari za nchi kavu katika nchi mbalimbali za kiafrika zaidi tujenge hapa Tanzania kwasababu Tanzania ndiyo kitovu itakayopelekea nchi nyingine zote zinazoizunguka Tanzania kama ambavyo Bandari ya Tanzania ni moja kati ya Bandari kubwa za east Africa”

“Tutafanya vilivyokuwa Bora hapa Tanzania ili iwe mfano wa kuigwa katika nchi zetu mbili”

Amesema kitengo cha uchukuzi na usafirishaji, ndicho kitengo kinachoweza kuunganisha siyo tu nchi ya Tanzania, bali nchi ya Tanzania na Bara Zima la Afrika hivyo aliwahakikishia watanzania kwamba nchi ya misri ipo tayari kufanya Kila ambacho kitaongeza mahusiano kati ya misri na nchi zingine za kiafrika.

Miongoni mwa Taasisi zilizowasilisha maeneo ya uwekezaji ni pamoja mamlaka ya usimamizi wa bandari TPA, shirika la reli nchini TRC,mamlaka ya viwanja vya ndege TAA, ATCL, TCAAA, DMI , NIT, TASAC , MSCL, TMA

About The Author

(Visited 41 times, 1 visits today)

Last modified: February 19, 2024

Close