Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaokwenda nchini Israel
kwaajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo, wazazi wao pamoja na wafanyakazi wa
Taasisi hiyo mara baada ya kuwaaga leo jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge ameishukuru Serikali ya Israel kupitia Shirika la Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) kwa kuendelea kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto wanaohitaji kufanyiwa upasuaji mgumu ambao haufanyiki hapa nchini.
Shukrani hizo amezitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akiwaaga watoto saba pamoja na wazazi wao wanaokwenda nchini Israel leo jioni kwaajili ya matibabu ya upasuaji mkubwa wa moyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge akizungumza na wazazi ambao watoto wao wanakwenda nchini Israel
kwaajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo wakati akiwaaga leo jijini Dar es Salaam.
Gharama za matibabu ya watoto hao saba na usafiri wa wazazi wao watano
pamoja na wataalamu wa JKCI wawili zinatolewa na Shirika la Okoa Moyo wa
Mtoto (Save a Child’s Heart – SACH) la nchini Israel.
Dkt. Kisenge alisema watoto hao wanaongozana na daktari bingwa wa moyo kwa watoto na muuguzi mmoja ambao watakuwa nao muda wote wa matibabu yao pamoja na kwenda kujifunza mambo mbalimbali kuhusu upasuaji huo ili watakaporudi hapa nchini waweze kuwahudumia watoto wengine wenye matatizo ya moyo.
“Kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe.Ummy Mwalimu nachukua nafasi hii kuzishukuru serikali za Tanzania na Israel kwa kufadhili matibabu haya ya watoto,”.
“Wenzetu Israel wametutangulia katika utaalamu wa upasuaji wa moyo kwani wameanza kufanya upasuaji kabla yetu, hivyo basi wanapokuja kufanya kambi za upasuaji wa moyo watoto ambao wanawakuta na matatizo yanayohitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi kuliko uliopo hapa nchini wanawachukuwa na kwenda kuwafanyia upasuaji huo nchini kwao”,.
“Gharama zote za usafiri wa watoto, wazazi wao na wataalamu wetu wa afya pamoja na matibabu zinagharamiwa na SACH, ninawashukuru sana kwa moyo wao wa upendo walionao kwa watoto wetu wenye matatizo ya moyo na hii yote inatokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali za Tanzania na Israel”,alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Deogratius Nkya ambaye anaambatana na watoto hao nchini Israel alisema wanatarajia kuondoka nchini leo jioni kuelekea Israel kwaajili ya matibabu ya watoto pia kujifunza mbinu mbalimbali za kuwahudumia watoto mara baada ya kurejea hapa nchini.
Dkt. Nkya alizishukuru serikali za Tanzania na Israel kwa kutoa nafasi ya kuwasaidia watoto pia kwa kutoa nafasi kwao wataalamu wa afya ya kuongozana na watoto hao kwani ni sehemu mojawapo ya kwenda kujifunza mbinu mbalimbali za upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kwa watoto.
Naye Jackline Patrick mmoja wa wazazi ambao wanaongozana na watoto wao kwenye nchini humo aliishukuru Serikali kwa kupata nafasi hiyo na kutoa kipaumbele katika kufanikisha kuwasafirisha watoto wao kwenda kupata matibabu nchini Israel.
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete inatibu magonjwa mengi ya moyo ya watoto kwa asilimia 90 kupitia wataalamu wazalendo waliopo. Hata hivyo wanamkataba na Israel kwa baadhi ya wagonjwa wachache ambao ni asilimia 10 wanaohitaji utaalamu wa hali ya juu zaidi kwenda kutibiwa nchii humo.
About The Author
Last modified: September 11, 2023