Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kutunza vifaa vya uandikishaji ili viweze kuendelee kuwahudumia wananchi.
Akifungua mafunzo ya watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa, Mkoani Morogorogo leo tarehe 18 Februari, 2025, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele amesema vifaa hivyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa na vinatarajiwa kuendelea kutumika kwenye maeneo mengine.
“Ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivyo kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hilo ambalo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Mnapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza,” amesema.
Akifungua mkutano kama huo mkoani Tanga, Makamu Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Rufani (Mst) Mbarouk Salim Mbarouk amewataka watendaji hao kufanya kazi kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hilo.
“Baadhi yenu mlibahatika kushiriki katika kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Tume ikiwemo uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika awamu zilizopita.
Kwa kutumia uzoefu mlionao na mafunzo mtakayopatiwa, ninaamini mtafanya kazi zenu kwa weledi, bidii na moyo wa kujituma ili kufanikisha zoezi hili,” Jaji Mwambegele amewaambia watendaji hao.
Amewataka kutumia uzoefu walionao kuwasaidia wenzao ambao hawakuwahi kushiriki katika zoezi kama hilo ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Uboreshaji wa Daftari utafanyika mkoani Morogoro na kwenye Mkoa wa Tanga katika Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli, Handeni, Pangani na Mkinga kwa siku saba kuanzia tarehe 01 hadi 07 Machi, 2025 ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa saa 02:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Zoezi hilo ambalo lilizinduliwa mkoani Kigoma mwezi Julai, 2024 limeshakamilika kwenye mikoa 27 ambayo ni Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma, Singida, Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, Kaskazini Pemba, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Mwisho.
*CAPTIONS*
INEC1228/ INEC1234/ INEC1239
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele ak
About The Author
Last modified: February 19, 2025