*Ataka isitumike kuchochea shari kama wanavyofikiri baadhi ya wanasiasa.*
Na Mwandishi Wetu, Kongwa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Stephen Wasira, amesema maana ya demokrasia ni majadiliano, hoja na maelewano kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano katika kujenga taifa.
Amesema demokrasia sio vurugu kama ambavyo baadhi ya wanasiasa hususan wa vyama vya upinzani wanavyofikiri na kupiga kelele kutaka shari jambo ambalo CCM haikubaliani nalo.
Wasira alieleza hayo leo wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ikiwa sehemu ya shughuli za kuelekea maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania ambao uliingiwa Aprili 26, mwaka 1964.
“Kama una hoja za kuwashawishi wapigakura wakukubali toa, kama huna kubali….kwa sababu hawana watu, uchaguzi wa serikali za mitaa wameshindwa kwa sababu hawana wagombea, sasa wanalalamika tumeibiwa mumeibiwa wapi?
“Vijijini humo hawana watu, hata mkienda kwenye kijiji cha Kongwa mkasema niitieni hata watu 10 wa CHADEMA nitakulipa, mtu atapata tabu sana na atakosa hela maana hawapo.
Alisema kutokana na kutokuwa na wananchi wanaowaunga mkono ndiyo maana wapinzani walishindwa kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Sasa wewe ukose asiliamia 60 ugombee asilimia 40, uweke watu hawana sifa, ushindwe halafu uende Umoja wa Mataifa, huko utaenda lakini sisi tutakuwa tumeshamaliza hiyo kazi.
Wasira alisema CCM ina ajenda ya kudumu ya kubadili maisha ya watu, yawe mazuri kila mwaka, ya leo yawe mazuri kuliko jana na ya kesho yawe mazuri kuliko ya leo.
About The Author
Last modified: April 24, 2025