Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya nchini kuelimisha wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi ili kulinda amani, heshima na mali zilizopo kwenye maeneo yao.
Kauli hiyo imekuja kufuatia tukio la hivi karibuni la wananchi wa Kata ya Murieti jijini Arusha kumpitisha Diwani kwenye madimbwi ya maji sambamba na Mwenyekiti wa mtaa wakidai viongozi hao hawajawajibika kutengeneza barabara hiyo ambayo ni adha kubwa wakati wa msimu wa mvua.
Akizungumza leo Desemba 18, 2024 kwenye uzinduzi wa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa Shule za Sekondari nchini iliyofanyika katika Shule Maalum ya Wasichana ya Sayansi ya Mkoa wa Dar es salaam iliyopo Manispaa ya Ubungo, Mhe. Mchengerwa amesema kitendo hicho si maelekezo ya serikali na wala sio utamaduni wa watanzania kuchukua Sheria mikononi.
Amesema Wakuu wa Mikoa yote ni Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa yao, hivyo wahakikishe wanakomesha tabia hiyo na wananchi wafuate taratibu zilizopo za kuchukua hatua kwa viongozi wasiowajibika.
“Chukueni hatua za kisheria mara wananchi wanapochukua hatua mikononi, hakikisheni amani na utulivu vinaimarishwa kwenye kila mikoa na Wilaya; wananchi wanapaswa kuwa na utii wa sheria na sio kuvunja sheria na linapotokea suala lolote la uvunjifu wa amani na wananchi wengine wakiona wenzao wamepongezwa wataona ni sawa na wataendelea kuchukia sheria mikononi kwenye maeneo yao na kuhatarisha uvunjifu wa amani,”amesema.
Aidha, amewataka viongozi wote kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka ofisini na kwenda kuwasililiza na kutatua kero za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
About The Author
Last modified: December 19, 2024