Visit Sponsor

Written by 9:47 am KITAIFA Views: 5

WAFUGAJI WANAOTOROSHA MIFUGO NJE YA NCHI WAONYWA

Wafugaji wanaotorosha mifugo yao kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu uliowekwa na
Serikali wametakiwa kuacha vitendo hivyo kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon
Pasua ameyasema hayo leo wakati alipotembelea mnada wa Themi maarufu ‘‘Lokii’’ uliopo
wilayani Arumeru kwa lengo la kutoa elimu kwa wafugaji kuhusiana masuala ya usalama
pamoja na kusikiliza changamoto zao.


Kamanda Pasua amebainisha kuwa jeshi hilo limebaini uwepo wa baadhi ya wafugaji kuchukua
vibali vya kusafirisha mifugo kwenda vijiji vilivyo karibu na mipaka ya nchi jirani lakini badala
yake wakifika maeneo hayo wanavuka mipaka na kwenda kuuza mifugo hiyo kinyume na
utaratibu.


ACP Pasua amewaonya wafugaji wote wenye tabia hizo kuacha mara moja kwani mifugo
pamoja na magari wanayoyatumia kusafirishia mifugo hiyo ikikamatwa itataifishwa na serikali
kwa mujibu wa Sheria.


Aidha Kamanda Pasua amesema Jeshi hilo kupitia misako na doria mbalimbali kwa kipindi cha
mwezi Aprili hadi Mei, 2023 limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 58 wakiwa na mifugo 325
kati mifugo 1,120 iliyoibiwa nchini kwa kipindi hicho.


Sambamba na hilo pia amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo kwa
kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuepukana na migogoro ya mara kwa mara ya wizi wa
mifugo na ile ya wakulima na wafugaji.


Msimamizi wa Minada kanda ya Kaskazini bwana Said Simba amebainisha kuwa ujio wa mkuu
huyo katika mnada huo umesadia wafugaji kupata elimu ambayo itapelekea kuhamasika katika
kulipa ushuru pamoja na kuepuka kutorosha mifugo kwenda nje ya nchi bila kufuata utaratibu.


Kwa upande wake Bwana Leyeyo Ngoipa ambaye ni mfugaji mbali na kushukuru kwa elimu
waliyopewa pia amewataka wafugaji kuacha kununua mifugo ya wizi na kuhakikisha pindi
wanapopeleka mifugo yao katika minada kuwa na nyaraka ambazo zitathibitisha uhalali wake.

(Visited 5 times, 1 visits today)

Last modified: May 30, 2023

Close