Jumuiya ya wafanyabiashara ya maduka Kariakoo, Dar es Salaam imezindua kampeni yenye jina la Mama Tuvushe 2025 yenye lengo la kumsapoti na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mambo mengi aliyofanya tangu aliposhika wadhifa huo ikiwemo kuwajali na kuwathamini wafanyabiashara nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Cate Hotel, Kariakoo, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa umoja huo, Martin Mbwana akiwa ameambatana na viongozi wengine wa Jumuiya hiyo alisema kuwa lengo la kuanzisha kampeni hiyo, ni kumuunga mkono mama kwakuwa amewafanyia mambo mengi, mazuri.
“Kwanza ni kwa ule uhuru aliotupatia wafanyabiashara wa Kariakoo, pili kwa huduma za kijamii ambazo anaendelea kuzifanya katika nchi yetu, hususani Dar es Salaam yetu, tatu ni uwekezaji ambao ameanza kuufanya kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam. Hivyo tumekubaliana kuwa na kampeni ya Tuvushe Mama 2025, tukiamini kwamba tuko na Mama, hatutamuacha Mama, kushikamana nae Mama hadi mwaka 2025 tutakapovuka salama katika uchaguzi mkuu,” alisema mwenyekiti huyo.
Aidha Mbwana alisema kuwa hivi karibuni kulikuwa na matatizo ya hapa na pale na namna ya ufanyaji biashara kwao ulivyokuwa na sintofahamu za hapa na pale, lakini kupitia uongozi wa Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Awamu ya Sita leo mfanyabiashara wa Kitanzania, wazawa wanafanya kwa uhuru.
“Leo Kariakoo ina amani, mfanyabiashara wa Kariakoo anafanya kwa uhuru na wamerudi kwa kasi kufanyabiashara, wageni wanakuja na nchi imefunguka. Kwa hiyo tunamshukuru sana mama, tunaishukuru Serikali yake kwa ujumla kwa sapoti kubwa waliyotupa ambapo leo hii tuna amani kubwa na Mamlaka ta Mapato Tanzania (TRA), tunafanyabiashara zetu vizuri na tunalipa kodi vizuri,” alisema Mbwana.
Vilevile alitoa ushuhuda kwamba hivi sasa huduma za kijamii ziko vizuri, kila mtaa inasambazwa lami, shule wanafunzi wanakwenda na zinajengwa tena za ghorofa, reli inajengwa, hospitali kuna dawa, mpaka hospitali za wilaya kuna CT Scan.
“Juhudi za mama yetu tunazitambua, tunamuunga mkono mama na tupo naye, naomba hilo alitambue na Watanzania wote wajue. Kampeni hii tumeianza leo, kwa niaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo na tutazunguka nchi nzima, wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa kuwaelezea wafanyabiashara wenzetu tumepata dhawabu ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye anapenda tukae kitako tusikilizane, ambaye aliahidi hataki kodi ya dhuruma, ambaye ameonyesha anawathamini wafanyabiashara na amefungua mipaka kwenye biashara. Tunaahidi na tumekubaliana kwa pamoja tumuunge mkono, tuvuke na Mama 2025,” Alisema Mbwana.
About The Author
Last modified: October 21, 2023