WAKATI haijulikani nini kinahitajika kufanyika hadi sasa tangu kuibuka kwa suala la uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia mwekezaji kutoka Falme za Kiarabu (UAE), uchumi wa nchi bado unahitaji kukua.
Kwa nyakati tofauti takwimu zimeonyesha namba zisizoridhisha kiutendaji katika bandari nchini ukilinganisha na uhalisia wa eneo la Tanzania linavyoweza kunufaika kupitia sekta ya bandari baharini na ziwani.
Hata hivyo, bado baadhi ya watu wanaamini kila uwekezaji ni wizi kwa mali ya umma. Bila kuangalia hali halisi kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Marekani na Uchina zinavyoruhusu kwa kasi ya ajabu uwekezaji kutoka nje.
Bandari ya Dar es Salaam ina historia ndefu tangu kuanzishwa kwake na Sultan wa Zanzibar katika miaka ya mwishoni 1800. Baadaye wakoloni wa Kijerumani na Kiingereza waliamua kuimarisha eneo hilo na kuwa bandari inayojiendesha kibiashara na kunufaika kwa kusafirisha abiria na mizigo hasa mazao ya biashara.
Hata hivyo, mwaka 1961 Tanganyika ilipopata uhuru bandari zote nchini zilikuwa chini ya wazalendo wakati huo serikali ikiongozwa na Rais Julius Kambarage Nyerere.
Ushindani ulikuwa mkubwa na mataifa jirani yenye bandari ikiwmo Kenya na Msumbiji. Lakini kijiografia bandari ya Dar es Salaam imekaa sehemu nzuri kupokea na kupeleka mizigo katika nchi kama Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na hata baadhi ya maeneo ya Kenya kutokana na ukaribu wake.
Mbali ya kuwepo fursa hiyo na ukubwa wa eneo lililopo kwa Bandari ya Dar es Salaam, bado haifui dafu kwa bandari za Afrika.
Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho alipata kuwaambia waandishi wa habari kuwa ndani ya mwaka bandari hiyo inapokea magari kati ya 250,000 hadi 300,000 ambapo zaidi ya asilimia 60 ya magari hayo yanakwenda nchi jirani.
โWatumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa wameongezeka zaidi, tunaunganisha nchi za maziwa makuu ambazo hazina bahari. Vilevile bandari yetu ni kiunganishi cha nchi za Mashariki ya Kati, Ulaya na Marekani,โ alisema Mrisho.
Hili si jambo la kulichukulia kirahisi, lakini mbali ya nafasi hiyo kiuchumi bado ufanisi upo chini hasa ikizingatiwa mahitaji yameongezeka ya nchi zinazohitaji huduma ya kupitishiwa mizigo.
Mathalani, takwimu zinaonyesha kuwa kwenye Bandari ya Dar es Salaam bila kuwepo mwekezaji katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kuanzia mwaka 2012/13 hadi mwaka 2021/22, shehena iliyohudumiwa katika imekuwa ikiongezeka kwa asilimia 5.14 kwa mwaka.
Ongezeko hilo ni kutoka tani milioni 12.55 za mwaka 2012/13 hadi tani milioni 18.41 za mwaka 2021/22.
Aidha, katika kupata maoteo kiwango cha ukuaji wa shehena kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita cha asilimia 5.14, kimetumiwa kupata matarajio ya shehena kwa kipindi kijacho cha miaka 10 kuanzia mwaka 2022/23 hadi mwaka 2032/33.
Katika kipindi hicho, shehena inatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 18.41 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 33.44 ifikapo mwaka 2032/33.
Maana yake akipatikana mwekezaji mwenye uwezo wa kuimarisha miundombinu ya kupakua na kupakia makasha, meli zitaongezeka na ufanisi utaongezeka na maana yake fedha pia zitaongezeka.
Unapozungumziwa ufanisi wa bandari katika viwango vya kimataifa ni pamoja na kupunguza muda wa meli kusubiri nje ya bandari, kupunguza muda wa malori unaotumiwa ndani ya bandari, kuongeza idadi ya mizunguko ya mashine ya kupakua na kupakia makasha.
About The Author
Last modified: October 19, 2023