Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetangaza kuwa ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro umefikia asilimia 27, huku ukitarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2026 kwa gharama ya shilingi bilioni 336.
![Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkama Bwire,](https://www.mwanahabaridigital.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image.jpg)
Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkama Bwire, akizungumza na wanahabari
Akizungumza Februari 6, 2025, wakati wa ziara ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na waandishi wa habari waliotembelea mradi huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA, Mkama Bwire, alisema bwawa hilo pia litasaidia kudhibiti mafuriko na kuwa chanzo cha uzalishaji wa umeme wa megawati 20, zitakazoingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Mradi huu mkubwa unatekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha huduma za maji na nishati nchini.
MANUFAA YA BWAWA LA KIDUNDA
Upatikanaji wa Maji kwa Uhakika: Bwawa hili litaongeza hifadhi ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na Pwani, hivyo kupunguza uhaba wa maji nyakati za kiangazi.
Kupunguza Mafuriko: Kwa kudhibiti mtiririko wa maji ya Mto Ruvu, bwawa litasaidia kupunguza athari za mafuriko ambazo huathiri jamii na miundombinu katika maeneo yanayopokea maji kutoka Ruvu Juu na Ruvu Chini.
Uzalishaji wa Umeme: Megawati 20 za umeme zitakazozalishwa zitasaidia kuongeza nguvu katika Gridi ya Taifa na kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara.
Maendeleo ya Kiuchumi na Ajira: Mradi huu umeajiri mamia ya watu katika sekta mbalimbali, na baada ya kukamilika, utasaidia shughuli za kilimo na biashara zinazotegemea maji.
Uhifadhi wa Mazingira: Kupitia udhibiti wa maji na mzunguko wake sahihi, bwawa litachangia katika uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza uharibifu wa ardhi na misitu.
Kwa maendeleo zaidi kuhusu mradi huu na miradi mingine ya kimkakati, endelea kutufuatilia
About The Author
bwawa DAR ES SALAAM dawasa kidunda mafuriko morogoro mradi ukame wananchi
Last modified: February 6, 2025