Visit Sponsor

Written by 5:55 am BIASHARA Views: 2

TIRA NA WADAU WAKE WAKABIDHI HUNDI YA MILIONI 321 KUUNGA MKONO MAADHIMISHO YA 61 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR



Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA na wadau wake Januari 7, 2025 wamekabidhi hundi ya mfano ya shilingi milioni 321 kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ikiwa ni mwitikio wa Sekta ya Bima nchini kuunga mkono Maadhimisho ya 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo kilele chake kitakua ni tarehe 12 Januari 2025 Gombani Stadium, Pemba.

Akipokea hundi hiyo ofisini kwake Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa shukrani za dhati kwa sekta ya bima nchini kwa hatua hii akisema mchango huo ni mkubwa na wanauthamini. Ameongeza kusema kuwa fedha zilizochangwa zitatumika kama ilivyokusudiwa. na kuwasilisha sekta ya bima kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na kwamba Serikali kupitia TIRA itaendelea kuweka mazingira weseshi kwa watoa huduma za bima.

“natoa wito kwa kampuni za bima nchini kuchangamkia fursa za Biashara zilizopo kupitia miradi inayoendelea Zanzibar na ofisi yangu ipo tayari kutoa msaada pale inapohitajika”

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Bima Tanzania, Bi. Khadija Said akiongoza ujumbe uliokabidhi hundi hiyo ameeleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi ya sekta  ya bima nchini ya kuwa sehemu ya maadhimisho hayo ili kuibua na kuchochea ushirikiano wenye tija na Serikali hususani kwenye miradi  mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini kuona namna kampuni za bima za nchini zinavyoweza kushiriki kwenye kukinga majanga.

Katika ujumbe huo pia Mwakilishi wa Umoja wa Kampuni za Bima Tanzania (ATI) Bw. Wilson Mnzava ambae pia ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya CRDB (CIC) ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikisha Kampuni za Bima katika tukio hilo muhimu “..huu ni mwanzo tu tunaahidi kwamba tutaendelea kushiriki kila mwaka ili kuhakikisha kwamba sekta ya bima nchini inakua ni miongoni mwa mafanikio ya maadhimisho haya”

Aidha, Bw. Wilson ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuendelea kutoa fursa kwa kampuni za bima za nchini ili ziweze kushiriki kwenye kukinga miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini ya serikali na wawekezaji binafsi.

About The Author

(Visited 2 times, 1 visits today)

Last modified: January 8, 2025

Close