Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezindua Siku ya Usalama Mtandaoni kwa semina ambayo imewakutanisha wadau mbalimbali iliyofanyika katika ukumbi wa ofisi za mamlaka hiyo jijini Dar es Salaam leo Februari 2, 2024.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mkurugenzi wa TCRA, Dkt. Jabiri Kuwe Bakari amesema kuwa siku hiyo huadhimishwa kila Jumanne ya pili ya mwezi wa Februari kila mwaka na huunganisha mamilioni ya watu ulimwenguni na kuhamasisha matumizi salama na yenye tija kwenye mtandao.

“Nawakaribisha katika semina hii muhimu iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ‘TCRA’ kwa wadau wote wa sekta ya mawasiliano inayofanyika kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya usalama mtandaoni ambayo ni mpango wa kimataifa uliyoanzishwa mwaka 2004 kwa lengo la kuhamasisha matumizi sahihi na salama ya mtandao wa internet,” amesema Dkt. Jabiri.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema kuwa semina hiyo ni kielelezo dhahiri cha hatua zinazochukuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania katika kuhakikisha elimu ya matumizi sahihi na salama ya mtandao na ili kuwafikia wadau wote wa sekta ya mawasiliano ambayo ndio rasilimali muhimu katika kujenga uchumu wa kidigiti ambao ukuaji wake unategemea sana matumizi chanya ya teknolojia.

“Dira ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ni kuwa na jamii iliyowezeshwa na huduma za mawasiliano kwa kuhakikisha usimamizi wa huduma ya mawasiliano unaoleta ustawi wa jamii ya Watanzania. Tunataka kuhakikisha huduma za mawasiliano inahakisi mambo matano.

“Kwanza huduma hizi zinapatikana kila mahali, nchi nzima mpaka kwenye visiwa na upande wa maziwa mpaka kwenye mipaka yetu, yaani kila mahali inapatikana, pili tunataka kuhakikisha huduma hizi ni bora, tatu tunataka kuhakikisha huduma hizi ni nafuu na zimuwezeshe kila Mtanzania aweze kunufaika nazo.
“Nne ambalo ndilo linatukutanisha hapa, tunataka tuhakikishe huduma hizi ni salama, tano na la msingi kabisa huduma hizi ziweze kubadilisha maisha ya Watanzania, zilete tija kwenye shughuli zetu za kiuchumi, kijamii na za kimaendeleo,” amesema Mkurugenzi huyo.

Vilevile Dkt. Jabir amesema kuwa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na maendeleo makubwa katika sekta ya Mawasiliano duniani na hapa nchini, Jamii kubwa ya Watanzania kote mijini na vijijini imefikiwa na huduma hii ya mawasiliano na kwamba anaamini wengi wamekuwa wakifuatilia taarifa ambazo TCRA imekuwa ikizitoa kila robo ya mwaka.
“Taarifa ya mwisho ambayo tumeitoa robo ya mwaka ambayo inaishia Desemba inatuonesha kwamba watumiaji wa internet kwenye nchi yetu imefikia takribani milioni 35.8 na idadi ya simu janja nazo zimefikia milioni 19.8, takwimu hizi zinaonesha udhibitisho wa ukuaji mkubwa wa matumizi ya internet,” amesema.

Dkt. Jabiri aliendelea, “Upatikanaji na unafuu wa huduma mbalimbali za mawasiliano nchini ni uthibitisho tosha kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga vyema kuandaa mazingira bora na wezeshi katika jamii ya Kitanzania na kuandaa Watanzania kushiriki ipasavyo kwenye uchumi wa kidigiti”.

About The Author
Last modified: February 2, 2024