Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bwa. Efrahimu Mafuru leo Septemba 24, 2024 amesema kuwa kuanzia tarehe 11-13 Oktoba, 2024 kutakuwa na onyesho kubwa litakalokwenda kwa jina la Swahili International Tourisim Expo (SITE 2024) litafanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam
Akiongea na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mkurugenzi huyo amesema onyesho hilo ambalo lengo lake ni kuimarisha network ya wafanyabiashara walio katika sekta ya utalii litashirikisha nchi zaidi ya 33 Duniani ikiwemo Tanzania.
“Moja kati ya mikakati ya Wizara ya Utalii ni kutangaza mazao yote ya utalii yaliyopo hapa nchini Tanzania na kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Utalii Kwa hiyo mwezi wa 7 tukatangaza kwamba tarehe 11-13 mwezi wa 10 kutakuwa na onyesho kubwa la SITE 2024”, amesema Mafuru.
Aiidha Mafuru amezitaja baadhi ya nchi zitakazoshiriki kuwa ni China, Denmark, Finland, Japan, Afrika Kusuni, Hispania, India, Urusi, Oman, Uholanzi, Nigeria, Brazil, Kenya, Ethiopia, Uganda na Lethoto.
“Tunato wito kama Bodi ya Utalii, Mhe. Rais alifanya kazi kubwa ya kutuzindulia filamu ya The Royal Tour iliyoifungua Tanzania na fursa nyingi za utalii na uwekezaji katika sekta mbalimbali za utalii, kazi yetu ni moja tu kutekeleza na kuendeleza pale ambapo Mhe. Rais amepaanzisha.
Aidha Mafuru aliitaja kauli mbiu ya onyesho hilo mwaka huu kuwa ni “Tembelea Tanzania kwa uwekezaji endelevu na utalii usiomithirika”, na kwamba hilo ndilo onyesho kubwa la utalii Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Vilevile Mafuru amesema kwamba katika onyesho hilo kutakuwa na jukwaa la uwekezaji, wamefanya mawasiliano na TIC (Kituo Cha uwekezaji) Ili wale wadau wanaohitaji kuwekeza katika Sekta ya Utalii waweze kupata
taarifa sahihi ambazo zitawawezesha wao kupata taarifa kwa urahisi zaidi.
“Tumewaalika pia mamlaka ya mapato nchini TRA, kutakuwa na mamlaka ya viwanja vya ndege, lakini pia kutakuwa na mabenki, Ili mtu aweze kujua kwamba ninawekeza Tanzania ni kodi zipi stahiki zilizopo katika Sekta ya Utalii na masuala ya kifedha yakoje pale.
“Lakini pia tutakua na ziara za mafunzo, tunaamini kwamba utalii huu sio tu wa kuuongelea kwenye vyombo mbalimbali vya habari, tunahitaji wadau mbalimbali waweze kupata uzoefu na tumeandaa maneno 6 ambayo mwaka huu tutawapeleka wadau mbalimbali kuweza kuwashuhudia”, amesema Mafuru.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi huyo amesema kuwa malengo yao mwaka huu ni Ukanda wa Kusini, Ukanda wa Magharibi na Zanzibar na kwamba utalii wa nchi hii siyo tu wa wanyama pori na siyo wa kanda moja, wanaionyesha Tanzania na mazao ya utalii katika kanda zote zilizopo nchini.
Mafuru pia ametoa wito kwa wadhamini kwakuwa kazi wanayoifanya ni kubwa, inabeba dhamira ya nchi katika Sekta ya Utalii, “Wengi mtakumbuka ya kwamba mchango wa Sekta y Utalii katika pato la Taifa Iko kwenye asilimia 17 na mchango wa Sekta ya Utalii kwenye fedha za kigeni ni zaidi ya asilimia 25 kwa hiyo huu ni mchango mkubwa, wadau watakaokuja watahitaji kuweza kushiriki katika mafanikio haya, kwa hiyo karibuni sana wadhamini, tunaendelea kuwafuata mmoja baada ya mwingine, yawepo mabenki, kampuni mbalimbali za simu, taasisi, jumuiya mbalimbali lakini pia mashirika ya umma ambayo yana uwezo wa kifedha, tunayakaribisha yaweze kuonyesha namna ambavyo wana sapoti juhudi za Mhe. Rais za kutangaza utalii huu. Karibu sana Mlimani City tarehe 11-13 mwezi wa 10 Ili tuweze kuleta mapinduzi katika Sekta ya Utalii hapa nchini Tanzania.
“Tusisahau zile hashtag zetu, #thesite2024 na #waitewaje255, kwa hiyo waendelee kuangalia katika mitandao mbalimbali ya kijamii, tuendelee kutag katika mitandao yetu Ili kuweza kupata taarifa zaidi za Nini kinaendelea katika Sekta hii ya utalii, Mlimani City mwezi wa 10 tarehe 11-13”, alisema Mafuru.
About The Author
Last modified: September 24, 2024