Visit Sponsor

Written by 5:37 pm KITAIFA Views: 5

TANESCO NA KANONA WAKUTANA KWA MAJADILIANO YA AWALI YA BIASHARA YA MAUZIANO YA UMEME

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI


📌 Wajadili  kwa hatua ya awali Sheria na makubaliano ya kuuziana umeme

📌TANESCO yaishukuru Serikali kuwa mstari wa mbele usimamizi wa miradi ya kimkakati ya umeme nchini



Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO ) limefanya mazungumzo ya awali kuelekea makubaliano ya  biashara ya mauziano ya umeme kati ya TANESCO na Kampuni  ya KANONA ya nchini Zambia.

Hayo yamesemwa na Meneja wa Maendeleo ya Biashara TANESCO Mha. Magoti Mtani katika kikao kazi cha majadiliano ya biashara ya kuuziana umeme kati ya kampuni hizo mbili.

Kikao hicho kilichofanyika Machi 17, 2025 jijini Dar es Salaam ambapo TANESCO inatazamia kufanikiwa kwa biashara hiyo kutaongeza na kuimarisha mapato ili kujiendesha kwa ufanisi.

“ Shirika limefanya mazungumzo na Kampuni ya Umeme ya  KANONA ya Zambia lengo likiwa ni kuangalia namna kampuni hizi zitakavyoweza kufanya biashara ya kuuziana umeme katika Ukanda wa Kusini ambapo pia biashara hii  inatarajiwa kufanyika kwa nchi zingine jirani huku sisi kama TANESCO, tukitarajia kuimarisha zaidi uwezo wetu wa kifedha “ amebainisha , Mha. Magoti.

Ameongeza kwa kuishukuru Serikali ya awamu ya sita ambayo imekuwa ikitekeleza miradi ya maendeleo ya kimkakati hususani miradi ya umeme na kwa kuwa mstari wa mbele katika kutoa ushirikiano wa kifedha kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati.

Naye , Mkuu wa Kitengo cha Biashara Kampuni ya umeme ya KANONA Bi. Nsofwa Sikanika ameeleza kuwa, kikao hiko cha majadiliano ya ushirikiano wa biashara hiyo ya umeme ni hatua za awali kuelekea kufanikisha utiaji saini makubaliano ya biashara hiyo ya kuuziana umeme unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni ambapo kukamilika kwake kutaruhusu biashara hiyo kuanza kufanyika rasmi kwa kampuni hizo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme na ukuaji wa uchumi kwa nchi za kiafrika.

Tanzania ni mwanachama katika masoko ya pamoja ya kuuziana umeme ya ukanda wa Afrika Mashariki ya (EAPP) na upande wa kusini mwa Afrika ya (SAPP) ambayo yatainufaisha Tanzania kuweza kuuza na kununua umeme kutoka nchi zingine za bara la Afrika.

About The Author

(Visited 5 times, 1 visits today)

Last modified: March 18, 2025

Close