Visit Sponsor

Written by 10:33 am KITAIFA Views: 8

SIMBACHAWENE AWASIHI WANANCHI KUTUNZA MIRADI INAYOTEKELEZWA NA SERIKALI MAENEO MBALIMBALI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akitoa maelekezo kwa Watendaji na Viongozi wa TASAF na wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Mkungo, Kata ya Bukome, Halmashauri ya Wilaya ya Chato ulifadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) chini ya Mpango wa OPEC awamu ya nne wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amewasihi wananchi
kuthamini na kutunza miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ya
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika maeneo yao kwa kuwa
ina lengo la kuondoa umaskini katika jamii.
Mhe. Simbachawene ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwa
nyakati tofauti na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na
Wananchi kwa ujumla katika Halmashauri za Wilaya ya Geita, Chato na
Bukombe Mkoa wa Geita.
“Nimetembelea na kukagua miradi iliyopangwa, kwa ujumla nimefurahi
sana kwa utekelezaji mzuri mathalani shule na vituo vya afya
vimejengwa kwa viwango vizuri. Hivyo, nitoe rai kwa halmashauri zote
nchini na wananchi kuhakikisha miradi hiyo inatunzwa kwa kuwa ni
sehemu ya chaguo na vipaumbele vya wananchi wenyewe katika
maeneo yao” amesema Mhe. Simbachawene.

Sehemu ya watumishi wa Kituo cha Afya cha Nyabilezi na wananchi wa Kijiji cha Nyabilezi, Kata ya Bukome, Halmashauri ya Wilaya ya Chato wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Geita.


Aidha, Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa moyo
mmoja ametoa fedha nyingi kupitia mpango huo ili ziwafike wanufaika
na wananchi kwa jumla kupitia miradi hiyo ambayo ni chachu ya
maendeleo. Hivyo, ameomba wananchi kuendelea kumuombea ili
aendelee kuwa na moyo wa huruma na unyenyekevu kwa maendeleao
ya wananchi wake.
“Umaskini si kukosa fedha tu, unaweza pia kuwa ni ukosefu wa elimu na
afya bora. Kwa kuwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mtu wa maono
amegusa sehemu hizo na kuhakikisha shule nzuri na vituo vya afya
kama vilivyojengwa mkoani Geita kupitia Mradi huo vinakamilika haraka
na kuanza kutumika” amesema Mhe. Simbachawene.
Vilevile, Mhe. Simbachawene amewasisitiza Waratibu wa TASAF katika
Mkoa wa Geita kuhakikisha shule na vituo vya afya vinavyojengwa
kupitia Mradi huo wa TASAF vinawekewa miundombinu ya maji na
umeme na kuweka madawati ili madarasa hayo yaanze kutumika.
Waziri Simbachawene amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu
iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani Geita na
kusikiliza changamoto zinazowakabili ili kuzitatua na kukagua miradi
inayotekelezwa na TASAF katika Halmashauri za Geita, Chato na
Bukombe katika Mkoa huo.

About The Author

(Visited 8 times, 1 visits today)

Last modified: September 16, 2023

Close