Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
DODOMA: Watumiaji wa bidhaa za mafuta ya petroli nchini wameuanza mwaka mpya wa 2025 kwa shangwe ya kuendelea kupata unafuu bei za bidhaa hizo kwa mwezi Januari 2025.
Taarifa iliyotolewa na EWURA, leo Jumatano, mosi, imeonesha bei za mwezi huu kuendelea kushuka ambapo petroli kwa lita imeshuka kwa sh. 105, dizeli kwa sh. 135 na mafuta ya taa bei imepungua kwa shilingi 15 kwa mafuta yaliyopokelewa bandari ya Dar es Salaam ikilinganishwa na bei za mwezi Desemba 2024.
Kwa upande wa mafuta yaliyopokelewa bandari ya Tanga, bei ya petroli pia imeshuka kwa sh. 105 kwa lita, dizeli sh. 136 na mafuta ya taa sh. 135 huku bandari ya Mtwara bei ya petroli kwa lita ikipungua kwa sh. 42, dizeli sh. 129 na mafuta ya taa sh. 157.
Ahueni hiyo inatokakana na kuendelea kuimarika thamani ya shilingi dhidi ya fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta nje ya nchi ambapo wastani wa kubadilisha fedha za kigeni umepungua kwa asilimia 11.27.
Ikumbukwe pia kwamba, bei za bidhaa za mafuta aina ya petroli zimeendelea kushuka mfululizo kwa takribani miezi mitano kuanzia mwezi Septemba 2024.
About The Author
Last modified: January 1, 2025