Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora imetoa rai kwa Taasisi Simamizi na Vyama vya Kitaaluma
kuhimiza na kuwasimamia watumishi kutoa huduma bora kwa wananchi
kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kupunguza
malalamiko kutoka kwa wananchi.
Rai hiyo imetolewa Jijini Dodoma na Mwakilishi wa Katibu Mkuu Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Felister Shuli wakati akifunga
kikao kazi cha siku mbili cha Watalaamu Waandamizi wa Taasisi Simamizi
na Vyama vya Kitaaluma kilicholenga kusimamia dhana ya utawala bora
katika utoaji huduma kwa wananchi.
Bi. Shuli amesema kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa
wananchi katika sekta ya afya, manunuzi, ujenzi pamoja na elimu ambayo
yanahusu uvunjifu wa maadili, hivyo anaamini mafunzo hayo waliyoyapata
kwa muda wa siku mbili yatasaidia kupunguza malalamiko kutoka kwa
wananchi.
Kufuatia hatua hiyo, Bi. Shuli amezitaka Taasisi Simamizi za Maadili na
Vyama vya Kitaaluma kujenga imani kwa wananchi na kuonesha thamani
ya fedha zinazowekezwa na serikali katika miradi mbalimbali kwa
kuwasimamia ipasavyo wataalamu wao katika utendaji kazi wao wa kila
siku
‘’Ni matarajio yetu kupitia mafunzo haya tutakuwa na utumishi uliotukuka
kwa kuwa na Watumishi wa Umma wenye kuzingatia weledi na wachapa
kazi ili kuendelea kulinda taswira nzuri ya serikali ’’ amesema Mwakilishi
wa Katibu Mkuu.

Sehemu ya Maafisa Waandamizi kutoka Taasisi Simamizi za Maadili na Vyama vya Kitaaluma wakiwa katika kikao kazi kilichofanyika kwa muda wa siku mbili jijini Dodoma kwa lengo la kusimamia dhana ya utawala bora katika utoaji huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Madilli kutoka Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Leila Mavika amesema kikao
kazi hicho kimewapa fursa ya kubadilishana uzoefu katika nyanja ya
usimamizi wa maadili katika utumishi wa umma pamoja na kujadili mikakati
mbalimbali itakayowasaidia kusimamia suala la maadili kwa watumishi wa
umma.
“Katika kuhakikisha suala hili linakuwa endelevu tumeweka mikakati ya
pamoja kwa lengo la kuhakikisha suala la maadili katika utumishi wa umma
linasimamiwa ipasavyo” amesisitiza Bi. Mavika.
Naye Afisa Muuguzi kutoka Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Bi.
Rehema Msanjila amesema mafunzo aliyoyapata yataenda kuleta
mapinduzi makubwa katika eneo analolifanyika kazi ikizingatiwa sekta ya
afya imekuwa ikilalamikiwa sana katika uvunjifu wa maadili.
“Nina imani kubwa kutokana na mikakati mikubwa tuliyojiwekea katika
kikao hiki, tunakwenda kuwa na wauguzi na madaktari wenye kuzingatia
maadili katika utoaji wa huduma kwa wananchi katika hospitali zetu hapa
nchini’ amesema Bi. Msanjila.
About The Author
Last modified: June 17, 2023