Bajeti ya dharura nayo yaongezezeka
Na. Catherine Sungura, Kigoma
Ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bajeti ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara za TARURA imeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 275 hadi Shilingi Bilioni 710.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri OR-TAMISEMI, Mhe. Zainabu Katimba wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Soko Kuu la Mwanga na Soko la Samaki la Katonga katika Manispaa ya Kigoma.
Mhe. Katimba alisema kwamba ongezeko hilo la bajeti ni sawa na asilimia 158.18 ambapo zinaenda kutekeleza miradi mbalimbali nchini.
Aidha, alisema kuwa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha maeneo mbalimbali ya nchi na kusababisha madhara makubwa kwenye miundombinu ya barabara kama vile mvua za El nino, kimbunga Hidaya, Mhe. Rais Samia aliongeza Bajeti ya dharura ya TARURA kutoka Shilingi Bilioni 21 hadi kufikia Shilingi Bilioni 254.3 sawa na ongezeko la asilimia 1,110.9 ya bajeti ya dharura.
“Mhe. Rais kwa kutambua kuwa barabara hizi zinaunganisha jamii zetu kwa kutoa huduma mbalimbali za kijamii na zinatumika kwenye usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za biashara na kupelekea kukuwa kwa uchumi wetu aliongeza Bajeti ya dharura ya TARURA”.
Aliongeza kusema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na mojawapo ya hatua zinazochukuliwa ni kuboresha miundombinu ya usafiri na usafirishaji.
“Msingi wa maboresho haya ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025, kama inavyofafanuliwa katika aya ya 57 ukurasa wa 82”, aliongeza Mhe. Katimba.
About The Author
Last modified: November 7, 2024