*๐ Lengo ni kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme*
*๐ Ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kilindi, Tanga waffikia asilimia 35.*
*๐Bilioni 2.63 kulipa fidia wanaopisha njia ya kusafirisha umeme Mkata- Handeni-Kilindi*
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya kusambaza umeme ili kuondokana na changamoto ya kukatika kwa umeme nchini.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 10, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Handeni Mjini, Mhe. Reuben Kwagilwa aliyeuliza ni lini Serikali itaondoa changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani Handeni.
“Changamoto ya kukatika umeme Wilayani Handeni inatokana na uchakavu na urefu wa miundombinu ya kusambaza umeme. Katika kukabiliana na changamoto hii Serikali kupitia TANESCO inaendelea na ukarabati wa miundombinu ya umeme ikiwa ni pamoja na kubadilisha nguzo za miti na kuweka za zege”. Amesema Kapinga
Ameeleza kuwa, Serikali kupitia mradi wa gridi imara inaendelea na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Mkata, Handeni ambacho kipo kwenye hatua za awali za ujenzi.
Ameongeza kuwa, ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Kilindi, Tanga umefikia asilimia 35 na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 kutoka Mkata kupitia Handeni hadi Kilindi umeffikia asilimia 30.
Akijibu swali la Mbunge wa Mlalo, Mhe. Rashid Shangazi aliyeuliza kuhusu Serikali kuona umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa vituo vya umeme vya Mkata, Lushoto na Kilindi kutokana na umuhimu wa vituo hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme Mkoa wa Tanga, Mhe. Kapinga amesema tayari Wizara ya fedha imeihakikishia Wizara ya Nishati kuwalipa wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa wakati ili waikamilishe.
Na kuhusu kusuasua kwa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkata hadi Kilindi kutokana na ulipwaji wa fidia, Mhe. Kapinga amesema fidia ya wananchi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkata, handeni hadi Kilindi ni takribani shilingi bilioni 2.63 ambayo Wizara ya fedha wameihakikishia Wizara ya Nishati kuilipa fidia hiyo.
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa, fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Mkata, Handeni tayari wameshalipwa fidia.
Akijibu swali la Mbunge wa Hanangโ, Mhe. Mhandisi Samwel Xaday aliyeuliza ni lini Serikali itatatua changamoto ya kukatika kwa umeme Wilaya ya Hanangโ, Mhe. Kapinga amesema Wilaya ya Hanangโ ipo katika mradi wa ujenzi wa gridi imara awamu ya pili ambapo kitajengwa kituo cha kupokea na kupoza umeme ambapo kwa sasa Serikali inaendelea na awamu ya kwanza ya mradi wa gridi imara.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Mhe. Grace Tendega kuhusu kukatika kwa umeme mkoani humo hasa Jimbo la Kalenga, Mhe. Kapinga amesema Serikali inayo mikakati ya kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Iringa ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya umeme kwa kubadilisha nguzo na nyaya chakavu.
Aidha, Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa kutokea Mkoa wa Iringa, Tunduma hadi Katavi Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa kusafilisha umeme wa TAZA ambao unahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme ambavyo vitaboresha upatikanaji wa umeme maeneo yote ya ukanda huo na kuongeza kuwa mradi huo utaunganisha gridi za Taanzania na Zambia.
About The Author
Last modified: April 10, 2025