Visit Sponsor

Written by 3:00 pm KITAIFA Views: 77

SERIKALI, BENKI YA DUNIA WAKUTANA KUJADILI MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Bi. Khadija Khamis Rajab, akifungua mkutano wa tatu wa kikao cha utekelezaji wa Tanzania ya Kidijitali kwa mwaka wa fedha 2023/2024  ulioanza februari 19-23 mwaka huu Mjini Zanzibar, Mkutano huo umewakutanisha Wataalamu kutoka katika Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wataalamu wa Taasisi za Umma pamoja na Benki ya Dunia (WB).

Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia-WB, wanaendelea na majadiliano ya namna
ya utekelezaji wa mradi wa Tanzania ya kidijitali, ambapo wataalam kutoka katika
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kutoka Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar
pamoja na taasisi mbalimbali za Umma, wamekutana mjini Zanzibar kwa ajili ya
majadiliano hayo.
Mradi huo unatarajia kutekelezwa kwa gharama ya dola za kimarekani milioni 150
sawa na shilingi Bilioni 348 za kitanzania na unatazamiwa kuboresha na kuimarisha
huduma za mawasiliano nchini. 


Ni katika mkutano wa tatu wa kikao cha utekelezaji wa Tanzania ya Kidijitali kwa
mwaka wa fedha 2023/2024 ulioanza februari 19 hadi 23 mwaka huu mjini Zanzibar,
ambapo pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili malengo ya kuongeza
upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti zenye gharama nafuu na ubora wa
juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi sambamba na kuboresha uwezo wa
serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bi. Khadija Khamis
Rajab, amesema matarajio ya serikali ni kwamba miradi ya kimkakati katika sekta ya
mawasiliano itatekelezwa.

Wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Taasisi za Umma pamoja na Benki ya Dunia wakiwa katika mkutano wa tatu wa kikao cha utekelezaji wa Tanzania ya Kidijitali kwa mwaka wa fedha 2023/2024  ulioanza februari 19-23 mwaka huu Mjini Zanzibar.


“Tunatarajia mradi huu utaenda kutekeleza mambo makubwa ili tuweze kutekeleza
miradi mingine ya kimkakati katika sekta yetu hii ya mawasiliano, tuna maeneo
mengi ya msingi ambayo yatakuwa yamegawanywa katika mradi huu wa Tanzania
ya kidijitali, na katika maeneo hayo kutakuwa na maeneo makuu matatu ambayo ni
pamoja na kupitia na kuhuisha sheria miongozo na taratibu za kisheria za TEHAMA
ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia” amesema Ndugu. Rajab.
Meneja wa mradi huo wa Tanzania ya Kidijitali Bw. Bakari Mwamgugu amesema pia
kutakuwa na maboresho ya miundombinu ya TEHAMA, ikiwepo kuunganisha taasisi
za serikali katika mkongo wa mawasiliano taifa, kuboresha vituo vya kuhifadhia
kanzidata, na kupeleka mawasiliano katika maeneo ambayo hakuna mawasiliano
ikiwa ni pamoja na kuboresha mawasiliano kutoka 2G kwenda 4G.
“Lengo la tatu ni kuboresha na kutekeleza mifumo mbalimbali itakayosaidia kutoa
huduma bora kwa wananchi na kwa wakati, ukiwepo mfumo wa jamii namba, ambao
kila mtanzania atatakiwa kuwa na namba moja tu ya kupata huduma” amesema Bw.
Bakari.


Mradi huo una malengo ya kuongeza upatikanaji wa huduma za mtandao wa intaneti
zenye gharama nafuu na ubora wa juu kwa serikali, wafanyabiashara na wananchi,
sambamba na kuboresha uwezo wa serikali wa kutoa huduma za umma kidijitali.

Mradi wa ‘Tanzania ya Kidijitali’ unaofadhiliwa na Benki ya Dunia unatekelezwa kwa
usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Pamoja na
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kushirikiana
na Taasisi mbalimbali zinazohusika na TEHAMA kwa upande wa Tanzania Bara na
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mwisho.

About The Author

(Visited 77 times, 1 visits today)

Last modified: February 19, 2024

Close