Visit Sponsor

Written by 1:22 pm KITAIFA Views: 8

SERIKALI, BENKI YA DUNIA KUENDELEA KUSHIRIKIANA KUBORESHA SEKTA YA AFYA



Na WAF Dodoma.

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amekutana na kufanya kikao na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika Bw. Daniel Dulitzky ambaye ameongozana na ujumbe wake akiwemo Bw. Nathan Belete, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia anayehudumu katika nchi za Tanzania, Zambia, Zimbabwe na Malawi.

Katika kikao hicho kilichofanyika leo Aprili 10, 2025 katika ofisi za Wizara ya Afya Jijini Dodoma, Waziri Mhagama ameipongeza na kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya Sekta ya Afya ikiwemo Progamu ya uwekezaji wa huduma za afya ya Mama na Mtoto (Tanzania Martenal and Child Health Investment Program – TMCHIP) wenye thamani ya Dola za Kimarekani Milioni 283.5.

“Ushirikiano baina ya Tanzania na Benki ya Dunia umekuwa ni wa manufaa makubwa unaosaidia katika maendeleo ya Sekta ya Afya nchini, tunaishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa msaada wa rasilimali fedha ambao umekuwa ukitumika katika kuboresha huduma za afya na ustawi wa afya ya jamii,” amesema Waziri Mhagama.

Waziri Mhagama amesisitiza kuhusu kuendeleza zaidi ushirikiano na msaada wa rasilimali kwenye utekelezaji wa Bima ya Afya kwa wote huku akieleza kuwa ni kipaumbele kikuu cha Serikali; Utekelezaji wa Programu ya Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii; pamoja na utayari wa kukabiliana na dharura na majanga.

“Tumejipanga kuwekeza kwenye mafunzo kwa wahuduma wa afya ngazi ya jamii zaidi ya 137,294 pamoja na kuwawezesha vifaa ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi, hivyo mkiwa kama washirika wetu wa maendeleo, msaada wenu ni wa umuhimu sana,” amesema Waziri Mhagama.

Awali akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, OR-TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange, Naibu Waziri OR-TAMISEMI amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili, Mwaka 2023 na 2024 programu ya TMCHIP imeweza kuajiri watumishi wa afya 1000 ambao wapo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ngazi ya msingi pamoja na kuboresha mfumo wa huduma za dharura na rufaa katika
Mikoa 26.

Kwa upande wake Bw. Daniel Dulitzky ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya Afya nchini yanayolenga kuboresha huduma bora za afya kwa wananchi na kusema kuwa Benki ya Dunia itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzana katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

“Tunaipongeza Tanzania kwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa zaidi ya asilimia 80 kutoka vifo 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/2016 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022 hii ni hatua kubwa sana,” amesema Dulitzky.

About The Author

(Visited 8 times, 1 visits today)

Last modified: April 10, 2025

Close