Visit Sponsor

Written by 4:36 am KITAIFA Views: 5

REA YAFIKISHA UMEME KWA WANANCHI 2400 NJOMBE

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI

Zaidi ya shilingi bilioni 80 zimetumika miradi ya REA Njombe

Wananchi watakiwa kutunza vyanzo vya maji

REA kuwezesha waendelezaji wadogo wa umeme kutoa huduma

Imeelezwa kuwa, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umepeleka umeme kwa wananchi wapatao 2,400 wa vijiji nane (8) vya Tarafa ya Lupembe, Wilaya ya Njombe mkoani Njombe baada ya kuiwezesha kampuni ya Matembwe Village Company Ltd kuzalisha umeme wa kilowati 550.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 30, 2024 na Mkurugenzi Teknolojia Mbadala na Nishati Jadidifu kutoka REA, Mha. Advera Mwijage alipotembelea mradi wa Matembwe Village Ltd unaomilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe pamoja na wananchi wa vijiji vya matembwe, Iyembela na Ikondo vilivyopo mkoani Njombe.

Amesema kuwa, mwendelezaji huyo ametoa  huduma kwenye vijiji nane (8) na jumla ya wateja 2,400 wameunganishwa ambapo kati ya hao, wateja wapatao 750 wameunganishwa kwa kuwezeshwa na Serikali kupitia REA.

“Gharama ambayo imetumika kuunganisha wateja ni takribani shilingi bilioni moja na REA inaendelea kumuwezesha kuunganisha wateja wengine ili wapate umeme wa uhakika, ” Amesema Mha. Advera.

Ameongeza kuwa, kwa sasa REA imefikisha umeme kwenye vijiji vyote nchini ingawa bado wananchi wanahitaji huduma ya umeme kwenye baadhi ya vitongoji na kaya ambazo hazijafikiwa na huduma hiyo.

“Mradi kwa sasa una zaidi ya miaka 30 na bado unaendelea kutoa huduma kwa ubora kwa kuongeza wateja wanaounganishiwa umeme, ” amesisitiza Mha. Advera

Vile vile, REA inaendelea kuuwezesha mradi huo kwa kutoa fedha ili wananchi wanaozunguka mradi wapate huduma ya umeme na kukuza shughuli za kiuchumi.

Kwa upande mwingine, Mha. Advera amesema zaidi ya shilingi bilioni 80 zimetumika kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya REA katika mkoa huo ikiwemo kuhakikisha maeneo yote ya vijijini yanafikiwa na nishati ya umeme.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Matembwe Village Company ltd, Johannes Kamonga amesema kampuni hiyo inahusika na kuzalisha umeme, usafirishaji na kusambaza umeme.

Ameongeza kuwa, kwa sasa kupitia mradi huo wanazalisha kilowati 550 za umeme kwa mashine tatu huku mashine moja ikizalisha kilowati 80, nyingine kilowati 120 na nyingine kilowati 350.

About The Author

(Visited 5 times, 1 visits today)

Last modified: October 31, 2024

Close