Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
-Amshukuru Rais Dkt Samia kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya Afya hapa Nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila kwa niaba ya waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mh Mohamaed Mchengerwa, leo Disemba 11,2024 amefungua kongamano la 39 la kisayansi la Kitaifa pamoja na Mkutano wa mwaka wa chama cha wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno katika ukumbi wa PSSSF Millenium Towers-Kinondoni.
RC Chalamila amemshukuru Rais Dkt Samia kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika katika awamu ya sita, hususani huduma za Afya ya Kinywa na Meno nchini hasa katika ngazi ya msingi, viti vya kutolea huduma za afya ya kinywa na meno (Dental chairs) 340, mashine za kidigitali za mionzi kwa huduma ya kinywa na meno (Periapical Dental X-rays) 306, mashine za mionzi za 2D-OPG zipatazo 57 na 3D-CBCT zipatazo 18 vyote kwa pamoja vimenunuliwa kwa gharama ya TZS 17,056,560,000 na watumishi 720 wameajiriwa kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya Kinywa na Meno nchini.
Aidha RC Chalamila ameipongeza Wizara ya Afya kwa kusimamia Mikoa na Halmashauri na kuhakikisha wanatenga fedha za kununua vifaa na Vifaa Tiba vya Afya ya Kinywa na Meno hivyo kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri kwenda Hospitali za rufaa za Mikoa, Kanda na Taifa kufuata huduma hizo. Haya yote yamefanyika ili kuimarisha na kufikisha huduma bora za afya ya kinywa na meno kwa Wananchi wa Tanzania katika maeneo yote Nchini.
Vilevile Mkuu wa Mkoa amesema tunapoelekea mwishoni mwa Mwaka 2024 ni vyema tukatambua kwamba kipaumbele Cha Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano Tanzania, pamoja na mambo mengine ni Mpango wa Bima ya Afya kwa wote yaani “Universal Health Insuarance”. Nichukue fursa hii kuwahakikishia kwamba, Kama nchi, tumejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya popote walipo na kwa wakati.
“Sote tunafahamu kwamba sheria ya utekelezaji wa mpango huu imeshasainiwa, hivyo basi, serikali inawategemea sana kama wadau muhimu katika kufanikisha dhamira yake hii ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya afya pasipo vikwazo vyovyote ninawasihi sana, kwa pamoja kama chama, na kila mmoja katika nafasi yake, tushiriki kikamilifu kuhakikisha mpango huu unaleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa letu, kwani Afya ya wananchi ni mtaji mkubwa” Alisema RC Chalamila.
About The Author
Last modified: December 12, 2024