MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umetoa msaada wa vifaa tiba kwa vituo sita vya afya ikiwa ni kuunga mkono juhudi kubwa wanazofanya watumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi kwenye maeneo tofauti ikiwemo eneo la utoaji huduma za afya.
Vituo vilivyonufaika na msaada huo ni pamoja na kituo cha Afya Kirumi kilichoko Wilaya ya Buatiama Mkoani Mara ambacho kimekabidhiwa leo Ijumaa Juni 30, 2023 na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF CPA. Hosea Kashimba.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kukabidhi vifaa hivyo, CPA. Kashimba alisema vituo vingine vitano, Mkunguni na Dimbani vilivyoko Kizimkazi, Zanzibar, Ikombe, Mtwara, Mji, Lindi na Ilembo Mkoani Katavi, vilikabidhiwa vifaa kama hivyo wakati wa kilele cha Wiki ya Uyumishi wa Umma iliyofikia kilele Juni 23, 2023.
“Hapa tuko mahala pake, nyote ni watumishi wa Umma mko hapa kuihudumia jamii ya wana Kirumi tunaamini vifaa hivi tulivyokabidhi vitasaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wagonjwa wetu.” Alisema CPA. Kashimba, ambaye alifuatana na Meneja wa Kanda ya Ziwa, Bw. Rajab Kinande, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wananchama, Bw. James Mlwoe na Meneja wa Mkoa wa Mara, Bi. Nyaswi.
CPA Kashimba liipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wake mahiri wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya afya nchini.
“Tunashuhudia maendeleo makubwa ya ujenzi wa miundombinu ya afya kila pembe nchini, ni wajibubwetu kama taasisi ya umma kuunga mkono mafanikio haya makubwa ya serikali.” Alifafanua Mkurugenzi huyo Mkuu wa PSSSF.
Akifafanua zaidi alisema, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) ilitoa maelekezo kwa taasisi za umma kuangalia namna bora ya kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kuwatemebea watumishi wa umma walio pembezoni mwa nchi ili kujua changamoto wanazokabiliana nazo katika kuwahudumia wananchi.
“Kubwa ni kuwasisitizia atumishi kuhusu uwajibikaji mahali pa kazi na eneo ambalo tulilichagua ni eneo la afya nah ii ni kwa kutambua huduma za afya ni moja ya mahitaji muhimu ya kila binadamu, kuimarisha utoaji huduma za afya ni kujenga jamii iliyo na afya bora na hivyo kupelekea kulinda nguvu kazi na hatimaye kuchangia uzalishaji na kuleta maendleo ya taifa.” Alifafanua.
Kwa upande wake, Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Mara, Bw. Msalika Makungu aliishukuru PSSSF kwa kuwaunga mkono kwa kutoa vifaa tiba.
“Tunaamini kwa msaada wenu kuwaunga mkono mnawatia nguvu si watumishi tu bali pia wananchi ambao kwa nguvu zao ndio waliojenga kituo hiki cha afya.” Alifafanua Bw. Msalika.
Alitoa wito kwa viongozi na wananchi kuvitunza na kuwa walinzi wa vifaa tiba walivyopokea.
“Hivi karibuni katika baadhi ya maeneo hapa nchini kumetokea wizi wa vifaa tiba kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya, na vifaa hivyo vinapoibiwa na watu wasio waaminifu wasiojali matokeo ya vitendo vyao kunakuwa na changamoto kubwa ya utoaji wa huduma.” Alisema na kuongeza….tuhakikishe yaliyotokea kwingine yasitokee hapa Kirumi, na kwa kufanya hivyo tunawapa nguvu na moyo hawa wanaotusaidia kwasababu wangependa kuona wananchi wanafaidika katika utoaji wa huduma.
Aidha Bw. Msalika aliwaomba wananchi kuwa walinzi wakuu kwani wahalifu hawawezi kufika kijijini bila ya kuwa na wenyeji.
About The Author
Last modified: June 30, 2023