Na Dr. Bravious Kahyoza na Michael Kihanga
Shughuli za mafunzo na uibuaji miradi iliyoanza tarehe 26/3/2025 inayoratibiwa na Kituo cha cha Ubia(PPPC) imeendelea wiki hii mkoani Katavi ambapo Halmashauri za Wilaya ya Mpimbwe, Mlele na Manispaa ya Mpanda zimefikiwa na jumla ya wataalamu 72 kupewa mafunzo.
Waratibu wa zoezi hilo, Dr. Bravious Kahyoza na Michael Kihanga wameyataja malengo ya zoezi hilo kuwa ni.
i.Kuelewa dhana ya PPP na kuibua miradi yenye sifa ya utekelezwaji wa ubia.
ii.Kuandaa maandiko dhana (Project Concept Notes)
iii.Kuandaa matangazo ya miradi kwa wawekezaji
iv.Kutumia teknolojia ya GIS katika uwekaji wa miradi kwenye ramani za Halmashauri
Aidha, kutokana na maandalizi mazuri ya Wakurugenzi wa Halmashauri hizo, watumishi na wataalam wengi wameitikia kwa wingi zoezi hili. Kwenye Halmashauri ya Mlele jumla ya wataalam 16 wamepatiwa mafunzo hayo. Halmashauri ya Mpimbwe wataalam 36 wamepatiwa mafunzo, huku wataalam 20 wakipatiwa mafunzo hayo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda.
HALMASHAURI YA WILAYA YA MPIMBWE
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Shamim Mwariko alieleza kuwa, Halmashauri yake ina fursa nyingi zinazoweza kuvutia ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma. Akifafanua kuhusu fursa hizo, amezitaja sekta za kilimo, utalii, michezo, biashara ya ndani na viwanda vidogovidogo kama sekta kinara kwenye mduara wa shughuli mama za kiuchumi.
Akichanganua dhana ya ubia kwenye faida zake kama kupata mitaji, teknolojia na ujuzi wa kimenejimenti; alisisitiza umuhimu wa kasi ya utekelezaji wa miradi ya mfano kwenye Halmashauri ili kuchochea mabadiliko ya fikra kwa watendaji.
“PPP inaweza kuwa na matokeo makubwa sana kwenye uchumi wetu, muhimu ni lazima kuwepo na mabadiliko ya fikra juu ya sekta binafsi. Sekta binafsi ni njia ya kubadili uchumi wetu” alisema Bi. Shamim.
Kwenye majadiliano ya uibuaji miradi kati wawezeshaji wa Kituo cha Ubia na wataalam Halmashauri, miradi kwenye maeneo ya kilimo, huduma za hoteli, michezo, masoko na miundombinu ya biashara ndogondogo yalionekana kuwa yenye kuwa nafasi zaidi ya fursa za ubia. Walau kwa hatua ya sasa.
Katika hatua nyingine, Bi.Shamim amepongeza jitihada zinazofanywa na Kituo cha Ubia na kushauri Kituo kuwa na mikakati endeleveu zaidi kwenye kuwa na vipaumbele vya miradi na maeneo ili kuchochea kasi ya ubia kwenye ujenzi wa uchumi wa hapa nchini.
Ameomba Kituo kutoa mafunzo zaidi kwa wataalam wa Halmashauri yake hasa kwenye maeneo ya uandaaji, kufanya maandiko na kuchambua miradi.
Amesisitiza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe itakuwa tayari muda wote kushirikiana na Kituo cha Ubia
HALMASHAURI YA MANISPAA YA MPANDA.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Bi. Sophia Kumbulu alilitaja zoezi hili kama ukombozi kwa Manispaa na mkoa kwa ujumla. Amesema Manispaa ya Mpanda kama mji mkuu wa mkoa wa Katavi una nafasi kubwa ya kuwa kiunganishi cha mkoa kwenye dhana ya ubia kwenye uchumi wa Katavi.
Akifafanua hilo, Bi.Sophia alisema:
“Manispaa ya Mpanda inaweza kuwa kitovu cha shughuli za ubia kwa mkoa wetu kwani hapa ni makao makuu na ndio lango lenyewe kwa nchi zinazotuzunguka kama DRC, Burundi na Rwanda”
Maeneo ya viwanda vya nguo, nyumba za wageni, masoko ya mazao, elimu, na michezo yaliibuka kama maeneo ya vipaumbele kwenye mapendekezo ya miradi yenye mvuto wa PPP.
Pamoja na shughuli za mafunzo na uibuaji wa miradi, wataalam wa Halmashauri waliopatiwa mafunzo hayo walitoa wito kwa Kituo kuendelea kuwa karibu na Halmashauri yao ili kuchochea shughuli za kiuchumi.
Manispaa ya Mpanda ambayo tayari ina miundombinu hitajika kama uwanja wa ndege wa Mpanda, barabara na nishati ya umeme, uko tuyari kupokea shughuli za ubia kwa kiwango cha juu.
HALMASHAURI YA WILAYA YA MLELE.
Halmashauri ya Wilaya ya Mlele chini ya uratibu maridhawa wa Mkurugenzi wa Halmashauri, Bi. Sigilinda Mdemu imelipokea zoezi hili la mafunzo ya dhana ya ubia kwa shauku kubwa.
Kwenye ufunguzi wa zoezi hilo kwenye Halmashauri yake, Bi. Mdemu alionesha kuwa fursa kubwa za ubia za ajili ya kuwakwamua wananchi, pamoja na sekta wezeshi za uchumi kama miundombinu, sekta ya kilimo na ufugaji, ni maeneo ya vipaumbele.
Bi. Mdemu aliyataja mazao ya kilimo na mifugo kuwa maeneo kinara ambayo wananchi wengi wanajishughulisha nayo na kuwa fursa za ubia zitakuwa nguzo kubwa kwenye kuongeza tija ya maeneo hayo.
“Pamoja na mambo mengine, hii ni Halmashauri ya kilimo na ufugaji na hivyo ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma unaweza kuwa na matokeo makubwa kwa uchumi wa wilaya na mtu mmojammoja” Alisema Bi Mdemu
Baada ya kupata mafunzo ya ubia, wataalam wa Halmashauri wakiongozwa na waratibu wa Kituo, waliibua miradi yenye uwezakano wa ubia kwenye ujenzi wa masoko ya mazao, maegesho ya magari, ufugaji wa nyuki na viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo kama karanga na tumbaku.
HITIMISHO
Mafunzo ya uibuaji miradi kwenye Halmashauri hizi tatu yameonesha mwamko na ari waliyonayo watendaji kwenye hatua za kubadisha uchumi wetu kupitia njia kuu ya kubadili rasilimali za asili kuwa rasilimali za kiuchumi kwa njia ya PPP.
Kwa muktadha wa menejimenti ya uchumi wa Halmashauri zetu nchi, hakuna shaka kuwa PPP ni njia ya uhakika ya kutimiza malengo 5 kwenye kuleta msawazo kwenye uchumi wetu kati ya serikali kuu na serikali za mitaa.
- Kugatua uchumi kwa kugatua mitaji. Kuondoa dhana ya uchumi kutokea juu na kuupeleka kwa wananchi.
- Kufanya wananchi wengi washiriki kwenye soko kwa njia ya kuongeza uwezo wa tija kwenye maeneo yao.
- Kuondoa dhana kuwa maeneo ya serikali za mitaa si kwa ajili ya uzalishaji bali ya utawala kama ilivyozoeleka.
- Kuondoa mwanya wa maendeleo kati ya miji na vijiji.
- Kukabiliana na kasi ya ukuaji wa deni la taifa kwa kupunguza mzigo kwa serikali kupitia ubia.
Ni kwa msingi huu, juu ya faida kuu tatu za ubia kwenye kuendesha miradi, yaani kupata mitaji, teknolojia na ujuzi wa kimenejimenti, hatua kama hii ya kituo cha ubia(PPPC) ni ya “jukumu la kihistoria” kwenye kubadili mfumo mzima wa uchumi wetu.




About The Author
Last modified: April 6, 2025