Na Lusungu Helela- Kigoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu amesema Kigoma sio Mkoa wa kupatia cheki namba (ajira) na kuhama kwa visingizio vya kuifuata familia au kwa sababu za ugonjwa huku akiwataka watumishi hao kuachana na dhana ya kuwa Mkoa ni wa pembezoni na hauna fursa za kiuchumi.
Mhe.Sangu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji, ikiwa ni kliniki ya kimkakati ya kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili Watumishi hao.
Amesema yeye kwa kushirikiana na Waziri wake Mhe. George Simbachawene wamelazimika kuweka utaratibu wa kufanya Klikini hiyo katika Mikoa mbalimbali nchini baada ya kuona Watumishi wengi wanalazimika kusafiri hadi jijini Dodoma kwa ajili ya changamoto walizonazo za kiutumishi ambazo zingeweza kutatuliwa papo kwa papo na Maafisa Utumishi wao.
Mhe.Sangu amesema kuna dhana imejengeka kuwa Mikoa ya Magharibi ikiwemo Katavi, Kigoma na Rukwa kuwa ni Mikoa ya adhabu kwa watumishi ambao wamepangiwa kufanya kazi katika maeneo hayo, jambo ambalo sio kweli hii inatokana na uboreshaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
‘’Kumekuwa na wimbi kubwa la Watumishi wa Umma mara tu baada ya kupata ajira huja kuripoti Mkoani Kigoma huanza taratibu za kuomba uhamisho, jambo hili sio sawa kwani wananchi wa Kigoma nao wanahitaji huduma bora kama wananchi wa Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.’’ Amesisitiza Mhe. Sangu
Amesema Mtumishi wa Umma atalazimika kuhama katika Mkoa huo endapo atakuwa amekaa miaka mitatu na kuendelea na pia kama atakuwa amepata Mtumishi mwenzake wa kubadilishana nae.
Hata hivyo, Mhe. Sangu amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu ametoa zaidi ya Trioni 11 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ikiwemo barabara na huduma mbalimbali ikiwemo za afya pamoja na elimu katika Mkoa huo.
Amesema kutokana na uboreshaji wa miundombinu hiyo kwa sasa Kigoma haina tofauti na Dodoma na Arusha kwani ina kila aina ya fursa pamoja na miundombinu mizuri
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Kirumbe Ng’enda amesema Kigoma inahitaji watumishi wachache lakini wenye utayari wa kufanya kazi katika Mkoa huo na sio wale walioletwa baada ya kufanya vibaya katika mikoa mingine.
Awali, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Mbwilo Elisante amesema Mkoa wa Kigoma unakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi kwani Watumishi wengi huhamishwa bila ya kuletwa mbadala.
About The Author
Last modified: November 16, 2024