Na. Lusungu Helela-Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Deus Sangu amesema suala la weledi katika kushughulikia mashtaka ya kinidhamu kwa Watumishi wa Umma nchini bado ni ya kiwango cha chini sana, hali inayopelekea Serikali kuingia gharama pindi rufaa na malalamiko ya mtumishi ambaye hakuridhika na uamuzi wa Mamlaka hizo yanaposikilizwa na kutolewa uamuzi na Tume ya Utumishi wa Umma.
Amesema Mamlaka hizo zimekuwa hazitoi fursa ya kujitetea kwa mtumishi mtuhumiwa kabla ya mtumishi huyo kuhukumiwa jambo ambalo ni moja ya misingi ya utoaji haki kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu na Sheria zilizopo.
Mhe. Sangu ametoa kauli hiyo leo Mkoani Dodoma mara baada ya kushuhudia usikilizaji wa rufaa na malalamiko ya baadhi ya Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi uliofanywa na Mamlaka zao za Ajira na Nidhamu katika maeneo yao ya kazi wakitoa utetezi wao mbele ya Makamishna wa Tume.
Amesema kamati za uchunguzi zinazoundwa zinapaswa kutekeleza wajibu wake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha taarifa zao za uchunguzi kubainisha iwapo makosa waliyoshtakiwa nayo watumishi watuhumiwa yamethibitika au kutokuthibitika kutendeka.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiiumiza Serikali kwa kuanza kulazimika kulipa mshahara Mtumishi katika kipindi chote alichokuwa amefukuzwa kazi au kusimamishwa.
Amesema mbali na gharama hizo ambazo Serikali hulazimika kuingia, pia katika hatua za mwanzo kabisa pindi Mtumishi anapotuhumiwa kuwa na makosa huanza mchakato wa kuunda kamati za uchunguzi ambazo wajumbe wake hulipwa posho ambayo ni fedha za Serikali.
Kufuatia hatua hiyo, Mhe. Sangu amesema anatamani kuona rufaa na malalamiko yanayopelekwa Tume ya Utumishi wa Umma yamalizika katika ngazi ya chini yakiwa yamefanyika kwa weledi pamoja na idadi yake kupungua ili Tume hiyo iweze kujikita kwenye masuala ya ukaguzi na mafunzo ili kuboresha ufanisi katika Utumishi wa Umma nchini.
Amesema kuwa mashtaka mengi yanayopelekwa Tume hiyo yamebainika kuwa na kasoro za wazi, hivyo kumpa nguvu mtumishi mtuhumiwa kuwasilisha rufaa na malalamiko yake katika Tume ya Utumishi wa Umma.
About The Author
Last modified: September 24, 2024