Visit Sponsor

Written by 3:56 pm KITAIFA Views: 33

NAIBU WAZIRI SAGINI APONGEZA WADAU KUCHANGIA VITENDEA KAZI JESHI LA POLISI

Kamati ya Usalama Barabarani imepongezwa kwa jitihada zake za kutafuta wadau na kulisaidia vitendea kazi jeshi la polisi nchini kitendo ambacho kinaliongezea ari na chachu katika utendaji wake.   

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi vilivyotolewa na wadau hao kwa Polisi wa Dar es Salaam leo Novemba 30, 2023, ikiwa pia ni hatua ya kuhitimisha wiki ya nenda kwa usalama barabarani, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Jumanne Sagini  ameipongeza kamati hiyo kwa jitihada inazofanya na kuiomba iangalie uwezekano wa kusaidia na katika baadhi ya mikoa mingine mikubwa kama Arusha, Mwanza Mbeya ili viweze kuimarisha usalama zaidi.

“Nazipongeza sana kamati zote kwa kubuni utaratibu wa kuhamasisha wadau katika kulisaidia jeshi letu la polisi ili kuongeza chachu ya utendaji na ninawapongeza wadau welevu kwa kukubali kushirikiana nanyi na kufanikisha kupatikana magari 10, pikipiki 20, bajaj 1, vipima ulevi 15, reflector jackets 400, raincoat 50 na taa za kuongozea magari 50, ni ubunifu wa aina yake”, amesema.

Aidha Naibu Waziri Sagini amesema kuwa vitendea kazi hivyo vimegarimu mabilioni ya fedha, kwa hiyo anawaelekeza wakuu wa Usalama Barabarani kusimamia matumizi na utunzaji wa vyombo hivyo ili viweze kuleta matokeo yanayotarajiwa katika kufanya operesheni zenye malengo ya kupunguza ajali za barabarani na kuongeza nguvu ya kutoa elimu ya Usalama Barabarani kwa kuwafikia watumiaji wa barabara wengi zaidi.

Awali kabla Naibu Waziri hajatoa pongezi hizo aliliomba jeshi la polisi limkutanishe na madereva bodaboda ili wabadilishane mawazo kuona namna ya kusaidia kupunguza ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikipoteza nguvu kazi kubwa ya Taifa na kusababisha ulemavu wa kudumu kwa baadhi yao, hasa kwa kundi hilo la bodaboda ambalo asilimia kubwa ni vijana.

“Wapanda pikipiki na abiria wao wavae kofia ngumu na tabia ya kubeba watu zaidi ya mmoja maarufu kama mishikaki iachwe, kila abiria akatae kubebwa mshikaki ili kupunguza hatari na madhara yatokanayo na ajali hasa zinapotokea. Kwenye hili nadhani mnitafutie jukwaa na vijana wa bodaboda, tukiongea nao Dar es Salaam tukaelewana huenda nchi nzima itaelewa, nachelea kutoa tamko hapa, wataumizwa, naomba mnikutanishe nao,” alisema Sagini.   

About The Author

(Visited 33 times, 1 visits today)

Last modified: November 30, 2023

Close