Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Naibu Katibu Mkuu – Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Ndg. Xavier Daudi ameipongeza TIRA kwa kuwa na Baraza la Wafanyakazi linalofuata misingi ya haki na utawala bora ambapo linatoa muda mzuri kwa Baraza kujadili mambo mbalimbali yanayohusu wafanyakazi kwa uwazi na uhuru.
Ndugu Xaver Daudi ambae ni Mgeni Rasmi wa Mkutano huo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Nne la Wafanyakazi la Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) unaondelea leo Disemba 4 mpaka 5, 2024 mjini Babati, mkoani Manyara. Mbali na hayo Naibu Katibu Mkuu pia amesisitiza maswala ya nidhamu, weledi pamoja na uwajibikaji kazini.
Awali akitoa neno la ufunguzi, Kamishna wa Bima Dkt. Baghayo Saqware alielezea mafanikio ambayo soko la bima nchini limeyapata kwa kipindi cha mwaka 2023 ambapo amesema uandikishaji wa ada za bima umeongezeka, lakini pia mchango wa sekta ya bima kwenye pato la taifa pia umeongezeka.
Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Bima Bi Khadija Said amemshukuru Mgeni Rasmi kwa nasaha zake ambapo ameahidi kuwa TIRA itaendelea kufanya kazi kwa kufuata misingi thabiti ya utumishi wa umma. Naibu Kamishna pia amemshukuru Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Bi Maryam Muhaji ambae katika neno lake ukaribisho alikaribisha Wajumbe wa Baraza kutembelea vivutio vya Utalii vilivyopo mkoani Manyara
Mkutano wa Baraza la Wafanayakazi wa TIRA unaoendelea unajadili mambo mbalimbali ya ustawi wa taasisi na wafanyakazi. Mada mbalimbali zinawasilishwa na kujadiliwa zikiwemo; utekelezaji wa Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 , utekelezaji wa kazi za Mamlaka kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka, Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, mada kuhusu kujenga uwezo wa matumizi ya TEHAMA pia mkutano utajadili hoja mbalimbali za wafanyakazi.
About The Author
Last modified: December 5, 2024