Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akionyesha moja ya jezi zitakazotumika kwenye EFD Marathon jana.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema kuwa katika kuhamasisha wakazi wa Dar es Salaam husasuni wilaya hiyo washiriki kikamilifu kwenye ulipaji kodi kwa kudai risiti na kutoa risiti kupitia mashine za EFD wameandaa shamrashamra kwa ajili ya hamasa hiyo waliyoipa jina la wiki ya EFD itakayoanza Septemba 23-30, 2023.
Akiongea katika mkutano na Waandishi wa Habari, ofisini kwake Ilala, Boma, Dar es Salaam jana, Mpogolo alisema kuwa lengo la kuwa na wiki hii ni kuhamasisha matumizi sahihi ya mashine hiyo, pili ni kujenga mahusiano kati ya Serikali na wafanyabiashara, wakiwemo wa Kariakoo.
“Tumekuwa wote ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Meneja wa TRA Mkoa wa Ilala, pia Meneja wa Kariakoo, sambamba na wafanyabiashara wa Kariakoo. Hii maana yake ni kujenga mahusiano mazuri kati ya walipa kodi kwa maana ya wafanyabiashara wa Ilala pamoja na ndugu zetu wa TRA, sisi serikali tukiwa ni kiunganishi kati ya pande hizi mbili.
“Lengo la tatu, tunaenda kwenye masuala ya kimichezo kwa maana ya kujenga afya zetu, hayo ndio malengo makuu tumeona tuyaweke katika wiki hii ya EFD. Wiki hii ya EFD tunatazamia kufanya yafuatayo, Septemba 23, 2023 tutakuwa na marathoni ya kilomita 10 na kilomita 5, tuko katika hatua za mwisho ila tayari medali pamoja na jezi za kukimbilia vimeshapatikana, ikiwemo njia tutakazopita,” alisema Mpogolo.
Aidha Mkuu wa Wilaya huyo wa Ilala alisema, katika mashindano hayo wanategemea kuwa na washindi watano kila eneo kwa wanawake na wanaume wote watapata zawadi, huku akihamasisha watu kuendelee kujisajili, kupitia website ya TRA, (www.tra.go.tz) na mpaka sasa zaidi ya watu 600 wameshajisajili kushiriki katika mashindano hayo.
“Zawadi nono zitatolewa, wale watakaojisajili mwanzo watapata jezi kwa ajili ya mashindano, ambayo itakuwa na maneno “EFD Marathon, Risiti yako ulinzi wako”. Mhe. Rais Dkt. Samia anafanya kazi kubwa sana, ili kuendelea kumlinda ni kuhakikisha unadai siti yako au unatoa risiti,” alisema.
Katika mashindano hayo mbio za kilomita kumi na kilomita 5 zitaanzia na kumalizika katika Uwanja wa Jakaya na kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo barabara ya Shaurimoyo, Machinga Complez, mtaa wa Lindi na kwingine, “Sisi watu wa Ilala ruti zetu ni katikati tu” alisema Mpogolo.
About The Author
Last modified: September 20, 2023