Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mjadala unaoendelea kuhusu uwekezaji kwenye bandari ya Dar es Salaam usiligawe Taifa kwa sababu Serikali ya awamu ya sita ni sikivu.
“Mjadala unaoendelea kuhusu bandari ya Dar es Salaam usitugawe Watanzania. Usipelekee tukasambaratika. Tusitumie nafasi hiyo kutugawa kiitikadi, kidini au kisiasa. Sisi ni wamoja na jambo letu ni moja. Serikali yenu sikivu itaratibu haya,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na mamia ya waumini waliohudhuria swala ya kitaifa ya Eid el Adh’haa iliyofanyika kwenye msikiti wa Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco, Kinondoni, jijini Dar es Salaam ambako alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Amesema Serikali inapokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau na kwamba ina nia njema kuhusu suala hilo na ndiyo maana ililiweka hadharani. “Natambua kuna watu wana hofu na umiliki wa bandari, ajira, ardhi na usalama wa Taifa lakini tusisahau kuwa TICTS wamekuwepo pale kwa miaka zaidi ya 22. Niwatoe hofu Watanzania kuwa malengo yetu ni kuboresha uchumi wa Tanzania. Tunataka watumiaji waliohama warejee,” amesema.
Amesema Tanzania imezungukwa na nchi nane ambazo hazina bandari na zinategemea bandari ya Dar es Salaam kupitishia mizigo yao. “Kwa hiyo bandari ya Dar es Salaam ni kitovu cha uchumi. Mwekezaji huyu ana uzoefu mkubwa na teknolojia ya hali ya juu katika uendeshaji shughuli za bandari kwenye nchi 68. Sisi pia tunatamani kufanya vizuri kama yeye alivyofanya katika nchi nyingine,” amesisitiza.
Amesema yeye binafsi kwa kushirikiana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wataongoza suala hilo la utoaji elimu na anaamini kwamba Watanzania wataelewa malengo hayo na hasa hatua ambazo Serikali inatamani kuzifikia.
About The Author
majaliwa Tanzania Waziri waziri mkuu
Last modified: June 30, 2023