Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii (JUMIKITA), Shaban Omari (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu kuwaunga mkono wafanyabiashara kwenye kampeni yao, Mama Tuvushe 2025, jijini Dar es Salaam Oktoba 24, 2023. Kushoto kwake ni Makamu Mwenyekiti wa Machinga Tanzania, Steveni Lusinde, kulia kwake bi baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara Kariakoo, pamoja na baadhi ya waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii nchini.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii (JUMIKITA), Shaban Omari amesema kuwa wameamua kuiunga mkono Kampeni ya Mama Tuvushe 2025 iliyozinduliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo hivi karibuni kwa lengo la kuifikisha mbali zaidi kwa kuyasema yote mema yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza katika ofisi za makao makuu ya JUMIKITA, Dar es Salaam Oktoba 24, 2023 huku akiwa sambamba na baadhi ya viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo pamoja na Makamu Mwenyekiti wa Machinga Taifa, Steveni Lusinde, Shaban alisema kuwa wao kama Wanahabari wa Mitandao ya Kijamii walilipokea wazo hilo kwa mikono miwili kwakuwa haliwezi kufika mbali kama halitapata sapoti ya media.
“Wenzetu hawa wafanyabiashara ambao kama mnavyojua wamepita kwenye misukosuko mingi mpaka kupelekea mgomo ambao baadae walikaa chini na Serikali na kuumaliza, kwa hiyo wakaona sehemu pekee ya wao kuonesha mshikamano wao na Serikali ni kuwa na kampeni ya Mama Tuvushe 2025 kwasababu wanaona tija ya kuwa huru kufanyabiashara zao. Lakini pia walisimamia kuhusu huduma za kijamii, wanaona jinsi Serikali inapambana kuweka vizuri miundombinu inayowazunguka ambayo imekuwa ikiwasaidia kupata riziki ya kila siku. Na sisi kama wanahabari wazo lao tumelipokea na kuliunga mkono,” alisema Shaban.
Aidha Mwenyekiti huyo wa JUMIKITA alisema kuwa, wao kama wanahabari wakishirikiana na wafanyabiashara hao pamoja na makundi mengine watachukua ujumbe wao na kuufikisha kwenye jamii kwasababu inataka kusikia mafanikio mengi yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita, kwakua sio kila jambo jamii inafuatilia, “Sisi tunaona tuna jukumu kubwa la kufikisha ujumbe huo, tutashiriki kwenye kampeni hii kwenye maeneo mengi na makundi mengi, kesho msishangae tukawa na vijana wa vyuo vikuu, keshokutwa mama ntilie au Umoja wa kina mama, lengo letu ni kuifikisha Kitaifa”, alisema Shabani.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Machinga Tanzania, Steveni Lusinde alisema walilipokea wazo hilo la Mama Nivushe 2025 kwa mikono miwili kwakuwa mama amewavusha kwenye mambo mengi kama wajasiriamali, kawapa wizara maalum (Jinsia na Wanawake), kwahiyo kampeni hiyo kwao ni kubwa kuliko hata watu wengine. “Lakini haikuishia hapo, Mheshimiwa Rais pia ameendelea kutengeneza bajeti mbalimbali kwenye kundi letu, lakini pia alitoa fedha kila mkoa milioni 10 za kuhakikisha Wamachinga wanapata ofisi. Kwahiyo sisi kama Wamachinga tuna kila sababu ya kuunga mkono hili wazo,” alisema Lusinde.
About The Author
Last modified: October 24, 2023