Visit Sponsor

Written by 2:55 pm KITAIFA Views: 34

MIKATABA YA UWEKEZAJI BANDARI IMEZINGITIA MAONI YA WATANZANIA – RAIS SAMIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema
Mikataba ya Uwekezaji wa Bandari iliyosainiwa imezingatia maoni yaliyotolewa kupitia
makundi mbalimbali ya kijamii, pamoja na sheria na taratibu zote za nchi.
Rais Samia amesema hayo leo wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba 3 ya uwekezaji
katika Bandari ya Dar es Salaam kati ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), serikali
na Kampuni ya DP World ya Dubai iliyofanyika Ikulu, Chamwino.
Aidha, Rais Samia amesema serikali ilisikiliza maoni mbalimbali yaliyotolewa na Chama
cha Wanasheria wa Tanganyika, vyama vya Siasa, asasi za kiraia, wanaharakati,
vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, viongozi wa dini na baadhi ya viongozi
wastaafu.
Vile vile Rais Samia amesema mikataba iliyosainiwa imetokana na makubaliano ya
awali kati ya serikali na Mamlaka ya Dubai ambao wameridhia mahitaji na matakwa ya
nchi kama yalivyoainishwa kwa kuzingatia maslahi ya taifa.
Mikataba iliyosainiwa ni Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Government Agreement);
Mkataba wa Upangishaji Ardhi (Lease Agreement) na Mkataba wa Uendeshaji wa
Bandari (Concession Agreement).
Rais Samia pia amesema uimarishwaji utakaofanywa kupitia uwekezaji huu utakuza
biashara za ndani na nje, pamoja na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani
hivyo kuongeza mapato ya serikali na kukuza uchumi wa taifa.
Mikataba hii 3 imesainiwa kwa kuzingatia Kifungu cha 2 cha Sheria ya Ubia Namba 6
ya mwaka 2023 (the Public Private Partnership Act Cap 103) na Kifungu cha 2 cha
Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 5 ya mwaka 2023 (the Public Procurement Act No
5 of 2023).

About The Author

(Visited 34 times, 1 visits today)

Last modified: October 23, 2023

Close