Visit Sponsor

Written by 3:34 am KITAIFA Views: 12

MAWAKILI WA SERIKALI TOENI USHAURI UNAOZINGATIA MASLAHI YA TAIFA

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akizungumza kwa njia ya mtandao na waajiriwa wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakati wa mafunzo elekezi yaliyofanyika mkoa wa Pwani.
Watumishi Wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wakimsikiliza kwa njia ya mtandao Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi wakati wa mafunzo elekezi yaliyofanyika mkoani Pwani.
Wakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Ditrick Luambano akichangia mada wakati wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wa Ofisi hiyo wakati wa mafunzo elekezi yaliyofanyika mkoani Pwani.

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI

Mawakili wa Serikali wametakiwa kutoa ushauri wa kisheria unaozingatia maslahi mapana ya Serikali na Taifa ili kuiwezesha Serikali kuokoa fedha zitakazosaidia kukuza uchumi kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

Wito huo umetolewa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi tarehe 24 Aprili 2025 wakati akizungumza na Mawakili wapya wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kwenye mafunzo elekezi yaliyotolewa kwa watumishi hao yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza na Mawakili hao kwa njia ya mtandao, Dkt. Possi amesisitiza kuwa Mawakili wa Serikali wana jukumu la kutunza siri wakati wote wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku katika uendeshaji wa mashauri ya Serikali ili kulinda maslahi ya Serikali na kuleta heshima ya taaluma ya sheria nchini katika kuhakikisha kuwa Serikali inapata haki yake katika kila shauri linalofunguliwa dhidi yake au linalofunguliwa na Serikali dhidi ya watu wasio na nia njema na Serikali.

Dkt. Possi alieleza kuwa OWMS ina jukumu kubwa la kuendesha mashauri yote ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali. Hivyo ni muhimu kwa Mawakili wa Serikali kufahamu vyema utamaduni wa Ofisi hiyo, muundo wake na namna inavyotekeleza majukumu yake. Pia, amewasihi wajenge mahusiano mazuri na taasisi nyingine zinazoshirikiana na OWMS mathalani Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama.

Vile vile, amewataka wawe na utamaduni wa kufanya utafiti wa kina wa kisheria kabla ya kuendesha shauri lolote la madai au usuluhishi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa utafiti unamuwezesha Wakili wa Serikali kujenga hoja imara, kuelewa mazingira ya kisheria na kujiandaa vizuri wakati wa usikilizwaji wa shauri.

Pia, amewasihi Mawakili hao kujenga tabia ya kujiendeleza kitaaluma ili waweze kuendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi katika maeneo maalum ya sheria mathalani sheria za kimataifa zinazohusu mafuta na gesi na zinazovutia wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza nchini kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha, amewasisitiza wajiendeleze hasa katika mazingira ya sasa ambapo sheria zinabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ili waweze kuwa na maarifa ya kisasa na ujuzi wa hali ya juu  katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya umma.

Aidha, Dkt. Possi amewahimiza Mawakili wa Serikali kuwa na nidhamu ya kazi kwa kuwahi kazini; kujenga mahusiano mazuri na watumishi wenzao; na kuepuka kuwa kikwazo kwa wengine katika utekelezaji wa majukumu kwa kuwa kuwahi kazini na kuwa na nidhamu ni misingi muhimu kwa watumishi wa umma katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, kuboresha utendaji kazi kwa kujenga heshima, uaminifu na ushirikiano mzuri mahala pa kazi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri na Udhibiti Ubora wa Ofisi hiyo, ndugu Camilius Ruhinda amesema kuwa Mawakili wa Serikali wapya wanapaswa kutambua kuwa wana jukumu kubwa la kuendesha na kusimamia mashauri ya madai na usuluhishi kwa mujibu wa sheria, weledi na kwa kuzingatia utii kwa mamlaka, pamoja na kuheshimu viongozi wao muda wote na mamlaka ya mahakama.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kuwa na muonekano nadhifu wa mavazi na mwenendo unaoakisi taaluma ya sheria na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ujumla.

Mafunzo hayo elekezi yamelenga kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali kuhusu namna Serikali inavyofanyakazi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa kufuata Sheria, Taratibu na Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma.

About The Author

(Visited 12 times, 12 visits today)

Last modified: April 25, 2025

Close