Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la
Shandong iliyopo nchini China na viongozi kutoka Wizara ya Afya walipotembelea
Taasisi hiyo jana kwaajili ya kuangalia maeneo ya kushirikiana kuboresha huduma
za matibabu ya moyo nchini.
Wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kushirikiana na
wenzao kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong la nchini China kuimarisha huduma
katika tiba ya upasuaji wa moyo upande wa kupandikiza mishipa ya damu,
matibabu ya mishipa ya damu iliyopasuka (dissecting aortic aneurysm), pamoja na
matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Peter Kisenge alipokutana na wajumbe kutoka Serikali ya watu wa
China walipotembelea Taasisi hiyo jana kwaajili ya kuangalia huduma
zinazotolewa na kujadili maeneo ambayo China itaendelea kushirikiana na JKCI.
Dkt. Kisenge alisema JKCI inaendeleza ushirikiano na Serikali ya Watu wa China
ambapo wataalamu mabingwa wabobezi wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali
ya Jimbo la Shandong wanatarajiwa kufika JKCI kubadilishana ujuzi na kuifanya
JKCI kuendelea kuwa kituo cha ubora Afrika Mashariki na Kati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter
Kisenge akizungumza na wageni kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong iliyopo
nchini China walipotembelea JKCI jana kwaajili ya kuangalia huduma zinazotolewa
na kujadiliana maeneo ya kushirikiana.
“Tumekutana na ujumbe kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong na kukubaliana
kuleta madaktari mabingwa waliobobea katika kutoa huduma za matibabu ya
moyo ambao wataenda kufanya kazi na JKCI kwa kipindi cha miaka miwili
kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa JKCI na kutoa huduma kwa wagonjwa
wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo”, aliesema Dkt. Kisenge.
Dkt. Kisenge alisema kupitia ushirikiano unaoenda kufanyika kati ya JKCI na
wataalamu wa afya kutoka Jimbo la Shandong la nchini China kutaenda
kuimarisha tiba utalii na kuifanya JKCI kuwa yakibingwa zaidi kwani kwa sasa
tayari ni Taasisi ambayo ni kituo cha ubora Afrika Mashariki na kati katika kutoa
huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo.
“Huko mbeleni tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Watu wa China kuimarisha
eneo la tiba mtandao (telemedicine) ambapo kwa pamoja tutaweza kumjadili
mgonjwa na kumpangia matibabu tukiwa maeneo mawili tofauti kurahishisha
matibabu ya wagonjwa wetu”, alisema Dkt. Kisenge
Kwa upande wake mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Dkt. Liggyle Vumilia alisema
Tanzania na China zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu mwaka 1968
kwa kutuma wataalamu wa afya Tanzania kwaajili ya kubadilishana ujuzi ambapo
hadi sasa wataalamu wa afya 11 kutoka nchini China wameshafanya kazi JKCI.
Dkt. Vumilia aliiomba Serikali ya Watu wa China katika kubadilishana ujuzi iangalie
namna ya kuwachukuwa wataalamu wa afya wa JKCI na kuwapeleka nchini China
ili wakaone namna wenzao wanavyotoa huduma kwani itawasaidia kubadili
mifumo waliyojiwekea na kuwa bora zaidi.
“Mkiwekeza katika Taasisi hii mmewekeza katika nchi nyingi za Afrika kwani sasa
nchi nyingi za Afrika zinaitegemea JKCI katika kutoa huduma za uchunguzi na
matibabu ya magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Vumilia
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Hospitali ya Jimbo la Shandong Dkt.
Mali Xin alisema Serikali ya Watu wa China imekuwa ikidhamiria kutoa huduma
bora na msaada kwa wagonjwa wa moyo waliopo Tanzania kwa kutoa wataalamu
wa afya mabingwa waliobobea katika magonjwa ya moyo.
Dkt. Mali Xin alisema ushirikiano uliowekezwa kati ya Tanzania na China
umeiwezesha JKCI kufanya upasuaji wa moyo wa aina mbalimbali na kupunguza
wagonjwa wanaoenda nje ya nchi kwaajili ya kutafuta matibabu.
“Kundi la 27 la wataalamu wa afya kutoka nchini China wakiwemo wataalamu wa
magonjwa ya moyo wanatarajiwa kufika nchini Tanzania karibuni, naamini kupitia
kundi la wataalamu hao watakaofika hapa JKCI litaenda kuwapa ujuzi mpya wa
namna ya kufanya upasuaji wa moyo mbalimbali”, alisema Dkt. Mali Xin
About The Author
Last modified: November 29, 2023