Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip
Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni ya
Kimataifa ya YARA wakiongozwa na Rais ambaye pia Mkurugenzi Mkuu wa
Kampuni hiyo Bw. Svein Tore Holsether, mazungumzo yaliyofanyika kando ya
Mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unaofanyika Davos nchini
Uswisi.
Katika Mazungumzo hayo, Makamu wa Rais ameihakikishia kampuni hiyo
kwamba serikali itaendelea kuiunga mkono katika kufanya shughuli zake
nchini Tanzania. Amesema dhamira ya serikali ni kuendelea kujidhatiti katika
kuwa ghala la chakula kikanda kwa kuzingatia ongezeko la watu pamoja na
mahitaji ya chakula.
Makamu wa Rais ametoa wito wa kuongeza ushirikiano zaidi baina ya
kampuni hiyo na Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo uwekezaji
katika miundombinu ya kilimo kama vile maghala, usafirishaji pamoja na
umwagiliaji. Pia amesema ushirikiano unahitajika katika kuimarisha kilimo
endelevu ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa na udhibiti wa maji.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema kampuni ya kimataifa ya YARA
inaweza kushirikiana na Tanzania katika kuwajengea uwezo wakulima wadogo
ili waweze kufanya kilimo cha kisasa na kuongeza uzalishaji. Pia
amewakaribisha kushirikiana katika tafiti za kilimo, kufanikisha masoko ya
mazao ya wakulima na kuongeza ushirikiano na wakulima na vyama vya
ushirika na taasisi zingine ili kufanikisha jitihada zilizopo.
Kwa upande wa Kampuni ya Kimataifa ya YARA imesema inaunga mkono
ajenda ya Afrika ya 2030 ambapo tayari imeweka mkakati wa kushirikiana na
mataifa mbalimbali yenye mpango wa muda mrefu katika kuimarisha usalama
wa chakula ikiwemo Tanzania. Kampuni hiyo imedhamiria kuongeza uwekezaji
nchini Tanzania na kuongeza ushirikiano katika kuwajengea uwezo wakulima.
Tayari kampuni hiyo inashirikiana na Mpango wa kukuza kilimo nyanda za juu
kusini (SAGCOT) katika kupima afya ya udongo nchini Tanzania.
Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu
Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Mbarouk Nassoro Mbarouk, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Natu
Mwamba pamoja na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Ofisi za Umoja wa
Mataifa Geneva Balozi Abdallah Possi. Kwa upande wa Kampuni ya kimataifa
ya YARA mazungumzo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa YARA kwa
Afrika na Asia Fernanda Lopez Larsen.
Kampuni ya Kimataifa ya YARA huzalisha na kusambaza mbolea, viatilifu vya
kilimo pamoja na kuwajengea uwezo wakulima.
About The Author
Last modified: January 17, 2024