Jumuiya ya Wafanyabiashara wa soko la Kimataifa la Kariakoo wamekubali kuendelea kufanya biashara katika soko hilo baada ya Serikali kuridhia kuendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakibili.
Wamefikia uamuzi huo leo (Jumatatu, Mei 15, 2023) baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kufika katika soko hilo na kuzungumza nao kufuatia mgomo ulioanza mapema Mei 15, 2023 ambapo walilalamikia masuala mbalimbali ikiwemo usumbufu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
“Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru, na kwa niaba ya wafanyabiashara, tumesikia maelekezo yako, lakini nilikuwa nakuomba sababu kesho kutwa tunakaa kikao, ningeomba kuwatangazia wafanyabiashara tukubali maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tumuunge mkono, tufungue maduka yetu na tukimaliza kikao cha kesho kutwa tunaamini kero zetu zote zitakuwa zimekwisha”
Awali Akizungumza na Wafanyabiasha hao, Mheshimiwa ameiagiza TRA kusitisha matumizi ya kikosi kazi ambacho kilikuwa kinafanya kazi ya ukusanyaji wa kodi katika eneo hilo “Task force hii ndiyo inaendesha kamatakamata kila siku, Kamishna wa Mapato ya Ndani wa TRA naagiza isitishwe, kanuni zipo, sheria zipo zinatuelekeza namna ya kulipa kodi, kamatakamata hii inafukuza wafanyabiashara Kariakoo na mbaya zaidi mnawakata hadi wageni kutoka nje”
Aidha, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa TRA wanaosimamia ukusanyaji wa kodi katika
eneo hilo na nchini kote kutekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya namna bora ya ukusanyaji wa mapato na kuacha kutumia nguvu wanapo tekeleza majukumu yao.
“Rais Dkt. Samia ameagiza kutolewa kwa elimu ya mlipa kodi, ili walipe kwa ustaarabu lakini kama unafuata kodi na mtu amejisahau, nenda kamkumbushe kwa utaratibu, kamatakamata inachangia kuua biashara na maduka mengi yatafungwa”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameahidi kukutana na wafanyabiashara hao Mei 17, 2023 kuwasikiliza na kutatua changamoto zao ili kuwa na suluhisho la kudumu .
About The Author
Last modified: May 30, 2023