📌*Ziara ya utalii ya Mabalozi kuchochea ushirikiano wa Tanzania na mataifa mengine
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuandaa ziara ya Mabalozi ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Zanzibar pamoja na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Aprili 11, 2025 jijini Dar es salaam wakati alipomwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa katika uzinduzi na ufunguzi wa ziara ya Waheshimiwa Mabalozi ya katika vivutio vya utalii.
“ Tanzania ni sehemu nzuri ya utalii duniani na ni imani yangu kuwa mtapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro ambao ni kivutio kikubwa duniani kwa wapanda milima, lakini pia tuna hifadhi ya wanyama ya Serengeti, Ngorongoro na sehemu zingine,” amesema Dkt. Biteko.
Ameongeza “ Mtatembelea pia Mji Mkongwe Zanzibar na pia mtaweza kujifunza maneno machache ya lugha ya Kiswahili kupitia ziara hii. Tuna maziwa na mito mingi na maeneo mengine ya kihistoria kama Bagamoyo na vijiji vya wamasai,”
Pamoja ma hayo, Dkt. Dkt. Biteko amesema Mabalozi hao wanatakiwa kuendelea kukuza ushirikiano na baada ya ziara hiyo watakuwa mabalozi wazuri wa utalii wa Tanzania.
Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Pindi Chana amesema leo ujumbe huo wa Mabalozi utatembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Ngorongoro, Serengeti na Mlima Kilimanjaro.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi amesema baada ya safari ya Arusha na Zanzibar, mabalozi wataendelea kuitangaza Tanzania kimataifa.
Balozi wa Comoro nchini na Kiongozi wa Balozi waliopo Tanzania, Mhe. Ahmada El Badaoui Mohammed Fakhi amesema kuwa kwa takribani miaka 11 aliyokuwepo nchini Tanzania hii ni mara ya kwanza kwa kuwa na tukio na namna hiyo.
“ Kwa niaba ya Waheshimiwa Mabalozi wote niipongeze Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje kwa kuandaa tukio hili,” amesema Mhe. Fakhi.
About The Author
Last modified: April 12, 2025