Visit Sponsor

Written by 6:25 am KITAIFA Views: 3

KAPINGA ASEMA KIPAUMBELE CHA SERIKALI NI KUFIKISHA UMEME KWENYE TAASISI ZOTE

Na Mwandishi Wetu

*📌 Taasisi 1,272 zaunganishwa na umeme  Lindi*

*📌  Maeneo ya pembezoni mwa miji kuendelea kuguswa na miradi ya umeme*

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha Taasisi zote zinazotoa huduma za kijamii, kiuchumi na kidini zinafikiwa na nishati ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya umeme Vijijini.

Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Aprili 11, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Maimuna Pathan aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha kupeleka umeme kwenye Shule na Taasisi zote zikiwepo za dini katika Mkoa wa Lindi.

“Hadi kufikia mwezi Machi 2025, jumla ya Taasisi  1,272 zimeunganishiwa umeme katika Mkoa wa Lindi zikijumuisha: Zahanati 259; Vituo vya Afya 42; Hospitali 9; Shule za Msingi 554; Shule za Sekondari 151; na Taasisi za Dini 257 (Misikiti 142 na Makanisa 115). “. Amesema Mhe. Kapinga

Ameeleza kuwa, kupitia miradi inayoendelea kutekelezwa na kusimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Taasisi 27 zinatarajiwa kupatiwa umeme mkoani humo..

Akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe, Mhe. Nicodemas Maganga aliyeuliza kuhusu Makanisa na Misikiti Mbogwe kutokuwa na umeme na mpango gani Serikali inao kuzipelekea Taasisi hizo umeme, Mhe. Kapinga amesema Taasisi hizo zitafikiwa na huduma ya umeme kupitia miradi ya Vitongoji inayoendelea katika Jimbo la Mbogwe,

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Dkt. Christina Mzava kwa niaba ya Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo aliyetaka kujua ni ipi kauli ya Serikali juu ya Kata ambazo hazijaunganishiwa umeme Kahama na Shinyanga, Mhe. Kapinga amesema Serikali ina mikakati ya kuweka miradi ya umeme pembezoni mwa miji ili wananchi waunganishiwe umeme kwa bei rahisi.

Awali, akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kishapu, Mhe. Boniphace Butondo juu ya lini vijiji 42 vilivyobaki vya Wilaya ya Kishapu vitapatiwa umeme, Mhe. Kapinga amesema Jimbo la Kishapu lina jumla ya vijiji 117 ambapo hadi kufikia tarehe 30 Machi, 2025 vijiji vyote 117 sawa na asilimia 100 vilikuwa vimekwisha unganishwa na huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Serikali.

Akijibu swali la Mbunge wa Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara aliyetaka kufahamu wananchi wa Nywamwaga, Sirari na Nyamongo ni lini wataanza kuunganisha umeme kwa bei ya shilingi elfu 27, Mhe. Kapinga amesema maeneo ya Vijijini yanaunganishwa na umeme kwa shilingi elfu 27 na kwa yale ya pembezoni ipo miradi mingine ya pembezoni mwa mji.

About The Author

(Visited 3 times, 3 visits today)

Last modified: April 12, 2025

Close