Visit Sponsor

Written by 6:30 am KITAIFA Views: 4

KAMATI TENDAJI YA MRADI WA SOFF YAKUTANA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MPANGO KAZI ULIYOIDHINISHWA.




Morogoro, Tanzania; 10 Aprili 2025.



“Moja ya masuala yatakayojadiliwa katika kikao cha pili cha Kamati Tendaji ya Utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa (SOFF)  ni pamoja na kutathimini utekelezaji wa mpango kazi wa mwaka 2024,  kupokea na kupitsha mpango kazi na bajeti kwa  mwaka 2025”.Alisema Dkt. Ladislaus Chang’a, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC)  wakati akifungua rasmi mkutano wa pili wa kamati hiyo katika Ukumbi wa hoteli ya Cate, Morogoro, tarehe 10 Aprili 2025.



Aidha, Dkt. Chang’a aliendelea kwa kuishukuru Kamati hiyo pamoja na Sekretarieti kwa kazi kubwa iliyofanyika katika kuhakikisha majukumu ya mradi kwa mwaka 2024 yanatekelezwa kwa ufanisi ikiwemo hafla ya uzinduzi wa mradi huo.



Dkt. Chang’a alifafanua TMA iliandaa mpango kazi wa utekelezaji wa maelekezo matano yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa Uzinduzi yakiwemo masuala ya utekelezaji wa shughuli za mradi kwa wakati na ufanisi pamoja na ushirikiano baina wa wadau wa Mradi.


Awali wakati wa ufunguzi, Naibu Mwakilishi Mkazi Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Ndg. Amos Manyama alisisitiza kuwa UNDP itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania,  TMA na Wadau wengine wa mradi kuhakikisha malengo ya SOFF yanafikiwa. Aidha aliendelea kusisitiza haja ya kuendelea kuimarisha ushirikiano na TMA katika kuimarisha huduma za haki ya hewa hata baada ya mradi.



Katika hatua nyingine, Kamati ilipokea na kuidhinisha Mpango Kazi wa mwaka 2025, taarifa ya hesabu kwa mwaka 2024 na Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Mradi.



SOFF ni Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuimarisha Uangazi wa Hali ya Hewa kwa Nchi zinazoendelea na Nchi za Visiwa vidogo. Lengo la Mradi ni kuimarisha huduma za hali ya hewa katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi ili kulinda maisha ya watu na mali ikiwemo kuboresha zaidi miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na kuhakikisha Tanzania inakidhi mahitaji ya wadau wa Kitaifa na Kimataifa. Mradi huu unatekelezwa kwa muda wa miaka minne kuanzia Julai 2024 hadi Desemba 2027.

About The Author

(Visited 4 times, 4 visits today)

Last modified: April 12, 2025

Close