Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiangalia namna ambavyo wataalamu wa afya wa JKCI Dar Group wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura wakati wa uzinduzi wa Kitengo cha wagonjwa wa dharura katika Hospitali hiyo leo jijini Dar es Salaam
Huduma za dharura kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo
zimeboreshwa kwa kuwekeza vifaa vya kisasa na wataalamu mabingwa wa
kutoa huduma hizo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya Dar
Group.
Kitengo hicho cha dharura Hospitali ya JKCI Dar Group sasa kimeimarishwa kwa
kuwekeza vifaa vyenye gharama ya shilingi milioni 760 ambavyo ni mashine za
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiograph – ECHO) na mashine
za kiwango cha juu za magonjwa ya dharura Advanced Cardiac Monitors,
Defibrillator, Emergency Trolley na Ventilator.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa kitengo cha wagonjwa wa dharura kilichopo Hospitali ya JKCI Dar Group leo jijini Dar es Salaam
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge
alisema tangu serikali ilivyoipa dhamana JKCI kusimamia Hospitali ya JKCI Dar
Group imeendelea kuimarisha huduma na kuongeza vifaa vya kisasa katika
kitengo cha magonjwa ya dharura.
“Tumeimarisha kitengo cha dharura kwa kuwekeza madaktari bingwa
wanaotoa huduma kwa wagonjwa mahututi wawili na kutoa mafunzo ya
namna ya kuwahudumia wagonjwa wa dharura kwa wataalamu wengine wa
afya wanaofanya kazi katika Hospitali hii”, alisema Dkt. Kisenge.
Kisenge ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alimshukuru Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
mchango wake katika uboreshwaji wa Hospitali hiyo kwa kuendelea kuwekeza
vifaa vya kisasa hivyo kusogeza huduma karibu na wananchi.
“Katika muendelezo wa kusogeza huduma kwa wananchi JKCI inaendelea
kupeleka huduma mikoani ambapo hadi sasa tayari tumeshatembelea mikoa
11 na kuona watu zaidi ya 7000 ambao wengi wao hawakuwahi kupata
huduma za kibingwa za matibabu ya moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Dkt. Angella Muhozya alisema tokea kuanzishwa kwa kitengo cha
dharura Hospitali ya JKCI Dar Group mwezi Desemba mwaka jana idadi ya
wagonjwa imekuwa ikiongezeka kutoka wagonjwa watatu hadi watano
ambapo sasa kitengo kinapokea wagonjwa tisa hadi 15 wanaohitaji huduma za
dharura.
“Kutokana na wingi wa wagonjwa tumeona kuna ulazima wa kuongeza
vitendea kazi na wataalamu wabobezi ili tunavyokuza huduma pia tuwe na
uwezo wa kumudu mahitaji yote yanayohitajika kutoa huduma kwa wagonjwa
wa dharura ndio maana Taasisi ikawekeza vyakutosha”, alisema Dkt. Angella
Dkt. Angella alisema huduma ya magonjwa ya dharura hapo awali ilikuwa
ikitolewa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) peke yake lakini baada ya
wataalamu wa afya kupata mafunzo ya kutoa huduma hiyo huduma za dharura
zinaanza kupatikana na maeneo mengine kama ambavyo sasa inapatikana
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.
“Kwasasa JKCI kuwa na wataalamu wabobezi wa kutoa huduma kwa wagonjwa
wa dharura ni hatua kubwa kwani wataalamu hao kwa nchi nzima sio zaidi ya
15 hivyo kuifanya taasisi yetu kuwa na viwango vinavyokubalika kimataifa”,
alisema Dkt. Angella
About The Author
Last modified: September 1, 2023