
Na Sixmund Begashe – Dodoma
Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kuongeza jitihada zaidi za kukabiliana na Wanyamapori wakali na waharibifu hususani Fisi katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na usalama.
Akizungumzia jitihada hizo Jijini Dodoma, Mkurugenzi Kitengo cha Uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACC) Fidelis Kapalata, amesema Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi tangu imeunda kikosi kazi maalum cha kupambana na Wanyamapori wanaoleta usumbufu kwenye makazi ya watu, imesaidia kutatua changamoto hiyo hususani Mkoani Simiyu.
SACC. Kapalata amesema kuwa, katika kikosi kazi hicho chenye Askari wa Uhifadhi 27 kwa kushirikiana na serikali za Halmashauri za Wilaya katika Mkoa huo pamoja na wananchi, wameweza kudhibiti Fisi zaidi ya 25 ambao walikuwa kero kubwa kwa wananchi.

“Napenda kutoa shukrani na pongezi kwa askari wetu waliopo uwandani, wananchi na Serikali za Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu, kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika katika kuwakabili Wanyamapori hao waharibifu, niendele kuwaomba wananchi kuendelea kushirikiana askari wetu katika zoezi hili, ili tuweze kufikia malengo yanayokusudiwa”. Amesema SACC. Kapalata
Aidha, SACC. Kapalata amesema kuwa hivi karibu kumeripotiwa uwepo na Fisi waharibifu katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyopo Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma, ambapo tayari Wizara imeshachukuwa hatua ya kupeleka kikosi kazi cha askari wake ambao wamesha weka kambi na kazi ya kuwasaka Fisi hao imeshaanza.

“Kuhusu taarifa ya uwepo wa Fisi hatarishi katika Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa Wilayani Kongwa, tumesha peleka askari wetu na tayari wameshaanza kazi ya kuwasaka Fisi hao ni imani yetu tutaitokomeza changamoto hiyo kwa mafanikio makubwa kama ilivyokuwa katika Mkoa wa Simiyu”. Aliongeza SACC. Kapalata.
Ikumbukwe kuwa, uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii umeendelea kuunga mkono jitihata za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama bila kubughudhiwa na Wanyamapori wakali na waharibifu, kwa kuchukuwa hatua mbalimbali hususan za matumizi ya teknolojia ya kisasa, kuunda kikosi kazi maalum kutoka kwa askari wa Taasisi zote zinazounda Jeshi la Uhifadhi, kuongeza vitendwa kazi, kuelimisha umma, kushiriana na wananchi pamoja na uongozi wa maeneo husika.
About The Author
Last modified: April 9, 2025