NA MWANDISHI WETU, ZIMBABWE
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk, Samia Suluhu Hassan amezisisitiza nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kumaliza Uhasama uliopo baina ya DRC na Rwanda chini ya mchakato wa Angola.
Tamko hilo limetolewa kwa niaba yake na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi alipomwakilisha kufungua Mkutano wa Viongozi Wakuu na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika jijini Harare Zimbabwe.
Rais Dk, Samia ambae ni Mwenyekiti wa Chombo cha Siasa, Ulinzi , na Ushirikiano wa Usalama wa SADC amefahamisha kuwa upo umuhimu wa kuandaa mikakati madhubuti itakayoainisha juhudi zinazoendelea za kijeshi Chini ya SAMIDRC na za kidiplomasia chini ya Angola zenye lengo la kumaliza mzozo huo.
Amebainisha kuwa hali ya Ulinzi na Usalama Mashariki mwa DRC bado haijatengemaa Kwani bado makundi yenye Silaha yanasababisha vifo,na kuzorota kwa utoaji wa huduma za Misaada ya kibinaadamu ,raia kupoteza Makaazi na Ongezeko la Idadi ya Wakimbizi.
Aidha ameeleza kuwa licha ya nchi za SADC kukabiliwa na changamoto ya kifedha ni lazima kusaidiana kukabiliana na changamoto ya Amani na Usalama kama ilivyoainishwa na Itifaki na Nyaraka nyengine muhimu za SADC.
Amesisitiza kwa nchi za SADC kuwa hazipaswi kusita katika kurejesha Amani ya DRC kwani bila kufanya hivyo suala la Amani halitakuwa endelevu.
Amezihimiza nchi za SADC kutoa kipaumbele kwa masuala hayo ili kuwa na Kanda yenye Amani,Maendeleo na Ustawi.
Rais Dk, Samia amefafanua kuwa wakati nchi za SADC zikiendelea kujadili hali ya Usalama wa Mashariki ya DRC ni vyema kukawekwa mifumo imara ya Ufuatiliaji na utekelezaji wa maazimio yanayoidhinishwa na Jumuiya mbalimbali za Kikanda ikiwemo yale ya Umoja wa Afrika(AU) na Umoja wa Mataifa (UN).
Ameeleza kuwa hatua hiyo itawezesha kupatikana kwa Misaada ya kifedha na kilojistik kwa wakati na kuongeza Ufanisi wa Misheni za SADC na kupunguza gharama.
Rais Dk, Samia amezishauri nchi za SADC kutumia majadiliano ya Mkutano huo kutoka na maazimio yatakayokuwa chachu ya kupatikana kwa Amani ya kudumu katika Ukanda wa SADC na kuwa ni ushahidi wa dhamira ya nchi hizo ya kuleta Amani Endelevu.
About The Author
Last modified: November 21, 2024