Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Ilala kimewaandikia barua wanachama wake sita kikiwataka kujieleza kwa madai ya kukiuka katiba ya chama hicho.
Akizungumza Aprili 9,2025 Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Ilala, Waziri Mwenyevyale, amesema wanachama hao wamekiuka katiba ya chama hicho kwa kuanzisha kundi la G55 alilodai kuwa linakwenda kinyume na matakwa ya chama hicho.
Amesema kulingana na kanuni za maadili za chama hicho ibara ya 3 (a) kupinga msimamo wa chama hadharani ni kosa.
“Kupinga maamuzi halali ya vikao vya chama hadharani kwa mujibu wa katiba ya chama chetu ni kosa. Inatakiwa mtu atumie vikao sahihi kupeleka hoja zake.”Kuanzishwa kundi hili ni usaliti, kukataa ajenda ni usaliti, naelekeza viongozi wa matawi na kata, G55 waliopo kwenye mkoa wangu waandikiwe barua za kujieleza kwanini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kupinga msimamo wa chama hadharani na kuanzisha kundi ambalo malengo yake kichama hayafahamiki,” amesema Mwenyevyale.
Mwenyekiti huyo amesema wanachama hao sita wanatakiwa kujieleza ndani ya siku 14 na kuwaelekeza makatibu wa majimbo kushirikiana na viongozi wa matawi na kata kuhakikisha wanasimamia maelekezo hayo.
“Tunamtaka Mbowe (Mwenyekiti mstaafu wa Chadema) ajitokeze hadharani aeleze msimamo wake juu ya kundi hili, ili wananchi na wanachama atuondoe kwenye mashaka,” amesema.
About The Author
Last modified: April 12, 2025