Visit Sponsor

Written by 7:59 pm KITAIFA Views: 19

BODI YA UTALII KUJA NA ONESHO LA SWAHILI INTERNATIONAL TOURISM EXPO SITE 2024

Na Madina Mohammed DAR ES SALAAM

BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imesema kuwa Onesho la Swahili International Tourisim Expo-SITE (SITE 2024) ambalo ni la Nane litafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 13 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 12, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TTB Ephraim Mafuru akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi rasmi wa onesho hilo ambalo amesema ni muhimu katika kuimarisha Sekta ya Utalii Nchini.

“SITE 2024 inaongozwa na Kauli Mbiu ambayo ni “Explore Tanzania for a Life Time Investment and Seamless Tourism Experience,” amesema Mafuru na kuongeza,

“Onesho hili limeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuleta pamoja wadau wa ndani na nje ya nchi kutangaza fursa za uwekezaji na vivutio vya utalii vya Tanzania,”

Mafuru amebainishwa kuwa wadau mbalimbali kutoka katika mnyororo wa thamani wa sekta ya utalii watashiriki na kwamba lengo kuu la onyesho hilo ni kuonyesha vivutio vya utalii na kuchambua fursa zilizopo ili kusaidia kukuza sekta hiyo.

“Onyesho la mwaka huu lina malengo mahususi ya kuwaleta pamoja wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuona jinsi ya kuzitumia fursa za utalii zilizopo. Pia tutakuwa na mikutano na semina za masoko na uwekezaji ambapo wataalamu watatoa mafunzo kwa wadau jinsi ya kuboresha huduma zao na kujitangaza kimataifa,” ameongeza Mafuru.

Mafuru ameendelea kueleza kuwa nchi jirani na za Afrika ni washirika muhimu katika sekta ya utalii, na wamealikwa kushiriki kwenye onyesho hilo. “Washiriki watajifunza jinsi ya kutumia fursa za utalii, kuzitangaza bidhaa zao, na kufahamu matarajio ya wateja wa kimataifa. Ni muhimu kwa watoa huduma za utalii nchini kujua namna bora ya kutangaza bidhaa zao, kama vile hoteli na vivutio, ili viweze kuvutia soko la kimataifa,” ameongeza.

Aidha, Mafuru amesema onyesho hilo pia litaleta fursa za kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya waendeshaji wa utalii wa Tanzania na wale wa kimataifa. Alisisitiza kuwa mikutano ya kibiashara itakayofanyika itasaidia kujenga mtandao wa kiuchumi na kuboresha huduma zinazotolewa ili ziweze kukidhi matarajio ya masoko ya nje.

“Onyesho hili pia litasaidia waendeshaji wa utalii wa ndani kuungana na wenzao kutoka nje, hasa kuhusu masoko kama vile Ulaya. Kupitia majadiliano ya moja kwa moja, watapata fursa ya kujifunza mahitaji ya soko hilo, ikiwemo aina ya vifungashio na huduma zinazohitajika,” ameeleza Mafuru.

Amebainisha kwamba Bodi ya Utalii imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mabalozi wa Tanzania duniani kote ili kuvutia watalii. Alipongeza juhudi za balozi wa Tanzania nchini Brazili kwa kuleta kundi kubwa la watalii kushuhudia vivutio vya Tanzania.

Ametaja hatua za kuhusisha waandishi wa habari wa ndani katika mikutano ya utalii, kama walivyofanya hivi karibuni katika hifadhi ya Mikumi, ili kuwapa uzoefu wa moja kwa moja na kuwajengea uelewa wa masuala ya utalii.

Ametumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa wadau wa ndani kuunga mkono jitihada za serikali, hususan zile zilizofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia filamu ya *Royal Tour*, ambayo imefungua milango ya utalii na kuonyesha fursa zilizopo nchini.

“Kazi yetu sasa, kama wadau wa sekta ya utalii, ni kuhakikisha tunatumia fursa hizi kupanua wigo wa mazao ya utalii, kukuza biashara zetu, na kuchangia katika maendeleo ya taifa,” amesema Mafuru.

About The Author

(Visited 19 times, 1 visits today)

Last modified: September 13, 2024

Close