Madaktrai Bingwa Wa Upasuaji wa Mifumo ya Fahamu, Ubongo na Uti Wa Mgongo (Neurosurgeons) watapewa mafunzo ya Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu kuanzia Oktoba 1-6, 2023 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma.
Akitoa taarifa kuhusu Mafunzo hayo, Dkt. Henry Humba, Bingwa wa Upasuajia wa Mifumo ya Fahamu Uti wa Mgongo na Ubongo BMH amesema mafunzo hayo yatahusu madaktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji wa Mifumo ya Fahamu, Uti wa Mgongo na Ubongo nchini.
“Tunatarajia kuwa na madaktari kutoka Hospitali za Benjamin Mkapa, Mnazi Mmoja NED Surgical Institute ya Zanzibar, Hospitali ya Mifupa (MOI), Mloganzila, Bugando, KCMC, Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Agha Khan” Alisema Dkt. Humba.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Prof. Akio Hyodo, bingwa mbobezi na Mshauri wa huduma za Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu ataongoza jopo la wataalamu wenzake wanne kutoka Japan.
“Tutaanza kwa mjadala wa kitaaluma utakaolenga kutathimini hali halisi ya utoaji wa huduma za Upasuji wa Mifumo ya Fahamu, Uti wa Mgongo na Ubongo nchini kulekea kwenye ujuzi wa juu wa utoaji wa huduma hizo” Alisema Dkt. Humba.
Mafunzo hayo yatakayodumu kwa siku tano mtawalia, yataongozwa na madaktari bingwa wabobezi wa Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu kutoka nchini Japan na watashiriki kufanya Upasuaji na madaktari wazawa ikiwa ni hatua za awali kuwezesha huduma hizo nchini.
Dkt. Humba amefafanua kuwa mafunzo hayo ni hatua za awali za Hospitali ya Benjamin Mkapa kuanza kutoa huduma za Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua ili Fuvu kushajihisha utalii wa matibabu nchini.
“Serikali ilikwisha leta vifaa ikiwemo mashine ya kuwezesha kufanyika kwa upasuaji, ikiwa na baadhi ya vifaa vinavyohitajika, kwa hiyo mafunzo haya ni hatua muhimu sana kwetu tunapoelekea kutumia mbinu hizo kutoa huduma” alisema Dkt. Humba.
Aidha, ujio wa Profesa Hyodo na Ujumbe wake ni maandalizi ya BMH kupokea mashine nyingine mpya ya kisasa itakayoimarisha utoaji wa huduma za Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu ikiwa ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Dkt. Higashiue Shinichi, Mwenyekiti wa Tokushukai Medical Corporation ambao ni wadau muhimu wa Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Upasuaji wa Mishipa ya Damu ya Ubongo bila kufungua Fuvu (kwa njia ya matundu) ni mbinu inayopunguza gharama za matibabu, muda wa kuuguza jeraha, muda wa daktari kufanya upasuaji.
About The Author
Last modified: September 29, 2023