Visit Sponsor

Written by 7:34 pm KITAIFA Views: 58

AGIZO LA WAZIRI MKUU LAMRUDISHA MWANAFUNZI ALIYEPOTEA MBEYA

Agizo alilotoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera na Kamati ya Usalama ya Mkoa huo wafanye uchunguzi zaidi na kwa haraka kuhusiana na tukio la kupotea kwa binti Esther Noah Mwanyiru ambaye alikuwa akisoma shule ya sekondari ya Panda Hill mkoani humo limezaa matunda, ambapo binti huyo amepatikana akiwa hai katika chumba cha muuza mkaa eneo la Ifisi mji mdogo wa Mbalizi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 23, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema chumba hicho alimopatikana binti huyo kinamilikiwa na Azurati Mohamed ambapo baada ya mahojiano alidai binti huyo alikabidhiwa na mmoja wa mteja wake.

“Amepatikana akiwa hai maeneo ya Isisi mji mdogo wa Mbalizi akiwa katika chumba cha mwanamke mmoja ambaye ni muuza mkaa kwenye nyumba ya kupanga ya Azurati Mohamed, alikabidhiwa na mtu mmoja ambaye ni mteja wake wa mkaa,”amesema

Aidha amesema mteja huyo anajulikana kwa jina la Baba Geofrey na kwamba baada ya makabidhiano hayo alisema amemwaribu mwanafunzi huyo hivyo akae naye siku mbili akimtafutia sehemu ya kumpangia.

Kwa upande wake Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi lilipomuuliza binti huyo iwapo anahitaji kwenda shule, alidai yupo tayari isipokuwa apelekwe shule nyingine.

“Nikipelekwa shule nyingine nitakuwa tayari kuingia darasani kusoma ila siyo shule niliyokuwa nasoma na naomba walimu wabadilike” amesema
Hata hivyo mkuu wa mkoa huo ameahidi kumpeleka kwenye shule yoyote ili aendelee na masomo.

Homela ameeleza kuwa katika vipimo vya awali walivyofanya havijaonesha kama binti huyo anaujauzito, na wanatarajia kufanya vipimo vingine.
“Ikibainika kwamba anaujauzito itatakiwa abaki nyumbani hadi ajifungue kisha arudi shuleni kuendelea na masomo,” amesema

Homela amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ikiwamo kumtafuta Baba Geofrey.

Waziri Mkuu alitoa agizo la kutafutwa mwanafunzi huyo Alhamisi, Juni 22, 2023 baada ya kupokea clip yenye maelezo ya mzazi wa binti huyo ambaye alikuwa akisoma kidato cha tano, tahsusi ya PCB kwenye shule hiyo.

Katika clip hiyo, Mama yake Esther anadai kwamba yeye na mume wake waliitwa na uongozi wa shule hiyo na kujulishwa kwamba Esther hajaonekana tangu asubuhi ya tarehe 18 Mei, 2023 na kwamba hadi sasa zimepita siku zaidi ya 20 wamekuwa wakimtafuta binti yao kila mahali lakini hakuna dalili za kumpata.

Mama Esther anadai kuwa Esther aliacha ujumbe wa maandishi akiwaaga rafiki zake na kuomba Mwalimu Jimmy aache kuwafanyia wanafunzi wengine kitendo alichomfayia yeye kwani kimesababisha maisha yake kuwa magumu.

“Naomba umfikishie salamu Mwalimu Jimmy, mwambie ameyafanya maisha yangu kuwa magumu sana hapa shuleni. Asiendelee kuwafanyia wanafunzi wengine kama alivyoyafanya maisha yangu mimi kuwa magumu,” alisema mama yake Esther akisoma sehemu ya ujumbe huo.

About The Author

(Visited 58 times, 1 visits today)

Last modified: June 23, 2023

Close