Visit Sponsor

Written by 2:11 pm KITAIFA Views: 4

NDANI YA WIKI MBILI UWANJA WA MKAPA UTAKUWA TAYARI KUCHEZEWA FAINALI

Na Mwandishi Wetu MWANAHABARI



Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma  amemuagiza mkandarasi anayesimamia ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuhakikisha maeneo muhimu ya uwanja huo yanakamilika ifikapo Mei 10, 2025.

Ametoa maelekezo ya ukarabati wa miundombinu mingine muhimu ndani ya uwanja huo, ikiwemo kukamilisha sehemu ya benchi la ufundi la waamuzi kwa kuweka mataili, kuweka viti vya muda katika sehemu zilizo wazi, na kuhakikisha ifikapo Ijumaa kazi hizo ziwe zimemalizika.



Agizo hilo amelitoa leo Aprili 29, 2025 katika ziara yake ya kukagua maendeleo ya ukarabati huo hususan eneo la kuchezea (pitch) ambalo linahitajika kuwa katika hali bora kwa ajili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba SC na RS Berkane.

Naibu Waziri Mwinjuma amesema  Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan imetoa maelekezo maalum kuhakikisha Watanzania wanashuhudia historia ya kipekee, kwani mara ya mwisho fainali ya CAF ilichezwa Tanzania ilikuwa ni mwaka 2023 ambapo Yanga SC walicheza fainali, na kabla yake mwaka 1993 Simba walifika hatua hiyo.



Mwaka huu, fainali hiyo itachezwa tena nchini na Simba watakuwa wenyeji wa mchezo wa marudiano Mei 25, baada ya kuanza ugenini Mei 17.

“Tunataka Watanzania wajivunie, wajione sehemu ya historia. Kombe linakuja hapa nyumbani na tunataka uwanja huu uwe tayari kulipokea,” amesema.



Ameongeza  kuwa, uwanja unapaswa kuwa tayari kwa watazamaji zaidi ya 63,000 kushuhudia tukio hilo la kihistoria, ingawa changamoto kubwa iliyojitokeza ni ubora wa sehemu ya kuchezea hasa baada ya mechi ya robo fainali kati ya Simba na Al Masry, hivyo eneo hilo linapewa kipaumbele cha ukamilishaji.

About The Author

(Visited 4 times, 4 visits today)

Last modified: April 29, 2025

Close