Na Mwandishi Wetu WAMACHINGA
-Akabidhi hundi ya zaidi ya Bilioni 5.5 kwenye vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo April 24,2025 amezindua utoaji wa mikopo ya 10% kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu Halmashauri ya Manispaa ya Temeke katika viwanja vya Mwembe yanga Jijini Dar es Salaam.
Akiongea wakati wa hafla hiyo RC Chalamila amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amewezesha mikopo hiyo isiyokuwa na riba kwa lengo la kuwainua kiuchumi wakazi wa Wilaya ya Temeke hivyo ni lazima mikopo hiyo irejeshwe ili kutoa fursa kwa watu wengine kupata mikopo hiyo.
Aidha RC Chalamila ametoa rai kwa wananchi wa Temeke kuacha kuilaumu Serikali isipokuwa watumie changamoto kuwa fursa ” Unakuta mtu anatoka kigoma pembezoni anakuja mjini anauza madafu kesho kutwa anakuwa mfanyabiashara mkubwa lakini mtu ni mzawa wa hapahapa Temeke anabaki kila siku kuilaumu Serikali ” Alisema Chalamila.
Vilevile RC Chalamila amepata fursa ya kutembelea mabanda mbalimbali ya wajasiriamali wanufaika wa mikopo ya 10% kujionea bidhaa zinazotengenezwa na wajasiriamali hao.
Kwa upande wa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe Abdallah Mtinika amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utoaji wa mikopo hiyo ambapo amesema kulikuwa na malalamiko ya kuchelewa kutoa mikopo lakini kilichochelewesha ni kuweka utaratibu mzuri ambao utawezesha uratibu mzuri wa mikopo ili wanaokopa waweze kurejesha kutoa fursa kwa wengine kuweza kuitumia fursa hiyo.
About The Author
Last modified: April 24, 2025